
IDARA ya Uhamiaji Nchini imefanya ukaguzi maalum nchi nzima kwa kipindi cha miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili, 2025 kwa lengo la kuwachukulia hatua za kisheria raia wa kigeni ambao wanaishi nchini bila kuwa na vibali au kufanya kazi/biashara kinyume cha masharti ya vibali vyao.
Taarifa ya leo Aprili 24, 2025 iliyotolewa na Msemaji wa Idara hiyo, SSI. Paul J. Mselle imeeleza kuwa kupitia zoezi hilo, Idara imefanikiwa kuwakamata jumla ya raia wa kigeni 7,069 kutoka katika mataifa tofauti na hatua mbalimbali zimechukuliwa dhidi yao ambapo raia 1,008 wamefikishwa Mahakamani huku kati yao 703 wakihukumiwa kifungo gerezani, 257 wamehalalisha ukaazi wao na watuhumiwa 4,796 wameondoshwa nchini wakati watuhumiwa wengine 305 uchunguzi bado ukiendelea.
Sambamba na hilo, Idara ya Uhamiaji kwa ushirikiano na Vyombo vingine vya Usalama wamefanya ukaguzi maalum katika eneo la Kariakoo ambapo jumla ya raia wa kigeni 62 kutoka katika mataifa mbalimbali wamekamatwa na kuondoshwa nchini kwa kosa la kuishi na kufanya biashara bila ya kuwa na vibali na baadhi yao kukiuka masharti yaliyoanishwa katika vibali vyao vya biashara.
Idara ya Uhamiaji imetoa wito kwa raia kigeni kuzingatia matakwa ya masharti ya vibali vyao ili kuepuka hatua za kisheria au usumbufu unaoweza kujitokeza wakati huu ambapo zoezi la ukaguzi linaendelea.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!