
Mchakato wa kumchagua Papa mpya, ni mchakato wenye muundo wa hali ya juu na wa siri unaofanywa na Baraza la Makadinali (College of Carfinals) katika Jiji la Vatican. Kuna hatua muhimu zinazohusika katika mchakato huu:
1. Nafasi ya Papa kuwa wazi: Mkutano huo maalum huitishwa kutokana na kifo au kujiuzulu kwa Papa aliyepita.
Papa anapokufa, Camerlengo (Chamberlain) mwenye mamlaka kutangaza rasmi kuwa kiti cha Papa kimebaki wazi “Sede Vacante” (kiti wazi), na maandalizi ya mkutano huo maalum yanaanza mara moja.
2. Kuwasili kwa Makardinali: Makardinali, ambao wanastahili kushiriki katika mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya (Conclave), wanakusanyika Roma. Kwa kawaida hukutana katika mfululizo wa Mkutano Mkuu ili kujadili mahitaji ya Kanisa na sifa zinazohitajika kwa Papa ajaye.
3. Kuanza kwa Conclave: Makadinali wanaingia katika Kikanisa cha Sistine (Sistine Chapel), ambapo wanakula kiapo cha kutunza usiri na hutengwa kabisa na ulimwengu wa nje wakati wote wa mchakato mzima. Hubakia ndani ya Mipaka ya Vatican hadi uchaguzi ukamilike bila kutoka, hata kama mchakato utachukua muda mrefu namna gani, hawawezi kuruhusiwa kutoka nje ya conclave.
4. Mchakato wa Kupiga Kura: Upigaji kura hufanyika mara kadhaa. Kwa kawaida kura hupigwa mara moja au mbili kwa siku, lakini idadi inaweza kuongezeka ikiwa ni lazima. Theluthi mbili ya wapiga kura inahitajika ili kumchagua Papa.
a. Upigaji kura: Kila kadinali huandika chaguo lake kwa Papa anayemchagua kwenye kadi ya mstatili, na kisha huikunja katikati. Wote husogea mbele ya Altare (Madhabahu) mmoja baada ya mwingine, ambapo hutamka kiapo na kuweka kura yake kwenye Kalisi maalum juu ya Altare hiyo. Baadaye, kura hukusanywa na kuhesabiwa, na matokeo hutangazwa.
b. Kuchoma Kura: Kura huchomwa baada ya kila duru ya kupiga kura. Iwapo hakuna atakayepata theluthi mbili ya kura zinazohitajika, kemikali maalumu huchanganywa kwenye karatasi za kura zilizopigwa kisha huchomwa moto katika tanuri iliyopo ndani ya Kanis ahilo ili kutoa moshi mweusi unaopanda juu ya dohani na kuonekana nje, kuashiria walio nje kwamba bado Papa mpya hajapatikana.
NB:
Tangu siku papa anapofariki, waamini na watu wengi kutoka ndani na nje ya jiji la Vatican na duniani kote hukusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican. Hubaki wakisali kumwombea Papa aliyefariki na kumwomba Mungu ili aangazie upatikanaji wa Papa mpya atakayeliongoza Kanisa.
Kwakuwa hawawezi kujua kinachoendelea kwenye uchaguzi ndani ya Sistene Chapel, kiashiria pekee wanachoweza kuona kujua mchakato umefikia wapi ni moshi mweusi (unaoashiria kwamba hajapatikana hivyo waendelee kusali), au moshi mweupe (unaoashiria waliopo nje kwamba Papa Mpya amepatikana).
5. Uchaguzi wa Papa:
Mara baada ya kadinali mhusika kupata theluthi mbili ya kura zinazohitajika, anaulizwa na Mkuu wa Baraza la Makadinali kama anakubali kuchaguliwa kwake. Iwapo atakubali, anajichagulia jina jipya kama Papa na mara moja anavishwa mavazi meupe ya Kipapa.
6. Moshi Mweupe:
Moshi mweupe ni ishara kwamba Papa amechaguliwa. Baada ya Mkuu wa baraza la Makadinali kupokea uthibitisho wa Papa mpya kukubali majukumu ya kuliongoza Kanisa, anatoka nje na kusimama katikati ya baraza (Balcony) ya Basilika ya Mtakatifu Petro na kutamka kwa lugha ya Kilatini “Habemus Papam” (Tunaye Papa).
Muda mfupi baadaye, moshi mweupe hupanda kutoka kwenye bomba la moshi lililowekwa kwenye paa la Sistine Chapel. Moshi huo hutengenezwa kwa kuongeza kemikali maalum kwenye kura zilizopigwa na huchomwa, na hivyo kutoa moshi wa rangi nyeupe badala ya nyeusi.
7. Kuonekana kwa mara ya kwanza na kutoa Baraka ya Kipapa:
Papa mpya aliyechaguliwa hujitokeza kwenye kibaraza cha juu (Balcony) na kutoa baraka zake za kwanza za kitume ziitwazo kwa Kilatini “Urbi et Orbi” (Kwa Jiji la Roma na kwa Ulimwenguni mzima), kwa waamini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro.
Na Elvan Stambuli, GPL
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!