

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetoa ufafanuzi wa habari zilizotolewa na Gazeti la Rada la tarehe 14.04.2025 kuhusu malipo ya Watumishi walioondolewa kwenye Utumishi wa Umma kwa kosa la kughushi vyeti na kubainisha kuwa habari hizo hazina ukweli wowote na kwamba zimelenga kuwachafua Viongozi na jina la Ofisi hiyo na kuleta taharuki kwa jamii
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Mary Mwakapenda imeeleza kuwa gazeti hilo limeandika kuwa Maelekezo aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za Mei Mosi mwaka 2022 hayatekelezeki.
Itakumbukwa, wakati wa Sherehe za Mei Mosi mwaka 2022 jijini Dodoma, Mhe. Rais Samia alielekeza watumishi walioondolewa kwenye Utumishi wa Umma kwa kosa la kughushi vyeti kurejeshewa michango yao waliochangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kwa msingi huo, watumishi waliokuwa wakichangia katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii PSSSF walistahili kurejeshewa michango ya asilimia tano (5) na waliokuwa wakichangia NSSF asilimia 10.
Kufuatia maelekezo hayo ya Rais, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma alitoa maelekezo kupitia barua yenye Kumb. CFC. 26/205/01”AT”/20 ya tarehe 31 Oktoba, 2022 kwa Waajiri wote katika Taasisi za Umma kutekeleza maelezo ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, maelekezo ambayo yametekelezwa kwa ufasaha na uadilifu.
Aidha, Mwanasheria wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye jina lake lilitajwa na Gazeti hilo, hakutafutwa wala kushirikishwa ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo kama ilivyoandikwa katika Gazeti hilo. (Tuseme limekiuka misingi ya uandishi wa habari).
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeuthibitishia Umma kuwa watumishi wapatao 15,288 walioondolewa katika Utumishi wa Umma kwa kosa la kughushi vyeti wameshalipwa michango yao yenye jumla ya Shilingi 47,020,753,222.23 na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF na NSSF kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!