
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepokea kesi ya jinai dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Antiphas Lissu, anayekabiliwa na shtaka la uhaini (treason) ambapo amesomewa shitaka hilo leo jioni.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani hapo, Lissu anadaiwa kutamka na kuchapisha maneno yanayodaiwa kuwa na nia ya kuchochea vurugu na kuvuruga uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Katika hati hiyo, inadaiwa kuwa tarehe 3 Aprili, 2025, ndani ya jiji la Dar es Salaam, Lissu alinukuliwa akisema:
“…walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli,… kwasababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hiyo ndiyo namna ya kupata mabadiliko… kwa hiyo tunaenda kukinukisha… sanasana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli… tunaenda kukinukisha vibaya sana…” imesema sehemu ya maandishi ya mashitaka ambayo Global Tv on line umeona.
Serikali inadai kuwa kauli hiyo inaashiria nia ya wazi ya kuchochea wananchi kuzuia uchaguzi na kuvuruga utulivu wa kitaifa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Mashtaka hayo yanaeleza kuwa Lissu, akiwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa kauli hizo akiwa na dhamira ya kuzuia uchaguzi na kuishinikiza serikali, hali inayodaiwa kuwa ni kitendo cha uhaini.
Kwa kawaida kesi ya uhaini huwa haina dhamana. Mwenyekiti wa zamani wa Chadema Freeman Mbowe aliwahi kushitakiwa na serikali kwa kesi ya uhaini na alikaa gerezani kwa zaidi ya miezi tisa kabla ya mkurugenzi wa mashitaka nchini kufuta kesi hiyo.
Na Elvan Stambuli, GPL
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!