HATIMAYE kocha Fadlu Davids amevunja ukimya baada ya kuondoka Simba na kwenda kujiunga na Raja Athletic, akieleza kila kitu alipofanya mahojiano exclusive na gazeti la michezo la Mwanaspoti.
Katika mahojiano hayo Fadlu alisema hajaondoka kwa kukurupuka bali alifanya makubaliano na uongozi wa Simba, kuwajulisha ofa aliyokuwa ameipata ya kurejea Raja ambako awali alihudumu kama kocha msaidizi.
Fadlu baada ya kuisimamia Simba katika mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) ikishinda huko Botswana bao 1-0 dhidi ya Gaborone United, hakurudi na timu Tanzania badala yake aliishia nyumbani kwao Afrika Kusini na kuanza safari ya kwenda Morocco kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kujiunga na Raja.
“Kila hatua ya kuwapo kwa ofa ya kutakiwa na klabu ya Raja niliujulisha uongozi wa Simba, hivyo nimemalizana nao kwa amani na nitaendelea kuheshimu ushirikiano wao kwa kipindi nilichoaminiwa kuifundisha timu na naamini pengine siku moja naweza kurejea,” alisema Fadlu na kuongeza;
“Naamini nimeacha msingi mzuri ambao utaendelezwa na kocha mwingine atakayekuja nyuma yangu, kuhakikisha Simba inafikia malengo yake kwa msimu huu, naamini itafika mbali katika michuano ya CAF na kupambania ubingwa wa Ligi baada ya msimu uliopita kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo.”
KUHUSU USAJILI
Kocha Fadlu alisema japokuwa aliwakosa baadhi ya wachezaji aliowahitaji kikosini akiwamo Feisal Salum ‘Fei Toto’ (aliyemaliza msimu uliopita na asisti 13 na mabao manne) na kiungo Balla Moussa Conte aliyejiunga na Yanga, alisisitiza Simba bado ina wachezaji wazuri.
“Bado Simba ina kikosi kizuri kitakachoibua ushindani dhidi ya timu pinzania, kikubwa waendelee kujituma na kuzingatia nidhamu ya kazi yao,” alisema Fadlu aliyesisitiza upendo wa mashabiki wa klabu hiyo utaendelea kuishi moyoni mwake.
Fadlu ameondoka na msaidizi wake, Darian Wilken na kocha wa makipa, Wayne Sandilands.
Ndani ya siku 444 sawa na miezi 14 au wiki 63 tangu aajiriwe Julai 5, 2024, Fadlu aliiongoza Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni baada ya miaka 31 tangu wekundu wa Msimbazi kucheza fainali ya kwanza katika michuano ya CAF.
Rekodi zinaonyesha kwa siku hizo, Fadlu ameiongoza Simba katika jumla ya mechi 53 za mashi-ndano yote, zikiwamo 30 za Ligi Kuu, 14 za Kombe la Shirikisho Afrika, moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tatu za Ngao ya Jamii na tano za Kombe la Shirikisho (FA).
Katika mechi 30 za Ligi, Fadlu ameshinda 25 kutoka sare tatu na kupoteza mbili, huku akifunga mabao 69 na kufungwa 13 akizoa jumla ya pointi 78, wakati katika mechi tatu za Ngao ya Jamii amepoteza mbili na kushinda moja, Simba ikifunga bao moja na kufungwa mawili.
Kwa Kombe la FA, Simba ilishinda mechi nne kati ya tano, huku moja ikipoteza katika nusu fainali dhidi ya Singida Black Stars na ilifunga jumla ya mabao 15 na kufungwa matano, wakati kwa Ligi ya Mabingwa imecheza mechi moja na kushinda kwa bao 1-0.
Kwa Kombe la Shirikisho Afrika ikifika fainali, Simba ilishinda mechi saba na kupoteza tatu na kupata sare nne ikiwamo ile ya fainali ya mwisho visiwani Zanzibar, huku ikivuna jumla ya mabao 15 na kufungwa 10. Hii ikiwa na maana katika mechi 53, Simba ya Fadlu ilishinda 38, kupoteza nane na sare saba na kufunga jumla ya mabao 101 na kufungwa 30 hadi anaiacha timu hiyo juzi ikiwa Botswana.
Upande wa mashindano ya ndani kwa msimu uliokuwa wa kwanza kwake na aliutumia kuijenga timu, hakupata taji lolote kwani alipoteza Ngao ya Jamii, alishika nafasi ya pili katika Ligi Kuu nyuma ya Yanga na ilitolewa katika nusu fainali ya Kombe la FA, japo aliifikisha timu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1.
“Mashabiki waendelee kuiunga mkono timu, ina nafasi ya kufanya mambo makubwa katika michuano yote msimu huu,” alisema Fadlu.
Credit:- MwanaSpoti
The post RASMI…..FADLU ATOA YA MOYONI KUSEPA SIMBA….ATAJA VIONGOZI…ISHU YA FEI TOTO….. appeared first on Soka La Bongo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!