
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema katika mikoa 11 ambayo tayari amefanya mikutano ya kampeni wananchi wameshasema kwamba watampigia kura za kishindo Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama hicho, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29,2025.
Dk.Nchimbi ameyasema hayo leo Septemba 21,2025 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni za Urais uliofanyika Mbambabay katika Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma ambapo ametumia nafasi hiyo kumshukuru na kumpongeza Dk. Samia kwa usimamizi mzuri wa rasilimali fedha ambazo zinatumika kuleta miradi ya maendeleo nchini.
Amefafanua katika kuomba kura alipangiwa maeneo ya kupita kama msadizi wake na mpaka sasa ameshapita mikoa 11. “Naomba nikupe salamu katika mikoa hiyo 11, imenituma nikuambie kwamba utashinda wewe (Dk. Samia) na CCM kwa kishindo katika mikoa yote 11.
“Wamenituma nikwambie, wabunge wa CCM watashinda kwa kishindo, madiwani wa CCM watashinda kwa kishindo na Rais wao kipenzi Dk. Samia Suluhu Hassan atashinda kwa kishindo,” amesema.
Aidha amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kumpendekeza kuwa mgombea mwenza wa Urais ambapo aliahidi kumsaidia kiongozi huyo kwa uaminifu.”Heshima hii siyo yangu pekee ni heshima kwa Mkoa wote wa Ruvuma, tunakushukuru sana.
“Nikuhakikishie kwa mila zetu Mkoa wa Ruvuma imani huzaa imani, nitakusaidia kwa uwezo wangu wote kwa uaminifu wangu wote kuhakikisha unatekeleza ilani ya CCM kama ulivyokusudia. Pia unafikia maono yako ya kulikomboa taifa letu kutoka hali duni kuwa hali bora Zaidi.”
Dk.Nchimbi pia amesema atakuwa msaidizi mwaminifu na kwa nguvu zangu zote huku akieleza kwa niaba ya wana Ruvuma wanamshukuru kwa maendeleo makubwa aliyoyafanya na siyo kwa Ruvuma tu bali Tanzania nzima.
“Uwezo wako wa kutafuta rasilimali, uwezo wako wa kusimamia mgawanyiko wake kuhakiksha kila pembe ya nchi yetu inapata rasilimali bila ubaguzi.Umetufanya CCM tusimame kifua mbele kukinadi chama chetu, uwezo wako umetupa heshima ya kuaminiwa na Watanzania ambapo kila kona tunapata ahadi za kishindo.
“WanaCCM wote, wananchi wote wa Mkoa wa Ruvuma tutahakikisha tunapiga kura za heshima kwa Rais wetu ambazo zitampatia nguvu kuendelea kututumikia ambazo zitawaonyesha dunia nzima kwamba tunaimani na mapenzi kwa Rais.”
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!