
Lilongwe, Malawi – Rais wa zamani wa Malawi Peter Mutharika (85) ameibuka kinara katika matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu uliofanyika Septemba 16, akiongoza kwa mara ya nne dhidi ya Rais wa sasa Lazarus Chakwera (70).
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (MEC) na makadirio ya shirika la habari la Reuters, Mutharika amejipatia takribani asilimia 51 ya kura halali katika mabaraza 9 kati ya 36, huku Chakwera akipata karibu asilimia 39.
Kisheria, mgombea anatakiwa kuvuka wingi wa zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kushinda moja kwa moja. Endapo hakutafikiwa kiwango hicho, duru ya pili italazimika kufanyika.
Wachambuzi wa siasa walikuwa wametabiri mapema kuwa uchaguzi huu ungelenga zaidi kwenye wagombea wakuu wawili pekee – Mutharika na Chakwera – wanaoongoza vyama viwili vikubwa zaidi bungeni.
Changamoto za Uchumi
Malawi imeendelea kushuhudia mdororo wa uchumi chini ya uongozi wa Chakwera, mchungaji wa zamani, aliyeingia madarakani mwaka 2020. Mfumuko wa bei umesalia juu ya asilimia 20 kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo. Aidha, kimbunga kikubwa na ukame vinavyohusishwa na mabadiliko ya tabianchi vimeharibu mazao na kuongeza ugumu wa maisha.
Historia ya Wapinzani
Mutharika, profesa wa sheria na rais wa Malawi kati ya mwaka 2014 na 2020, anakumbukwa kwa sera zilizodhibiti mfumuko wa bei na kuboresha miundombinu, lakini pia alikumbwa na shutuma za upendeleo wa kisiasa – madai aliyoyakanusha.
Kwa upande wake, Chakwera aliahidi kupambana na ufisadi alipoingia madarakani, lakini amekosolewa kwa madai ya kusuasua na kuchagua kesi za kushughulikia.
Usimamizi wa Uchaguzi
Tume ya Uchaguzi (MEC) imetahadharisha wagombea na vyama vya siasa kutojitangazia ushindi mapema, ikibainisha kuwa inakagua upya kila karatasi ya matokeo ili kuhakikisha usahihi. Matokeo ya awali kamili yanatarajiwa kutolewa ifikapo Septemba 24.
Historia ya uchaguzi nchini humo bado inatanda; Mahakama ya Katiba iliwahi kufuta ushindi wa Mutharika katika uchaguzi wa mwaka 2019 kutokana na kasoro, hatua iliyosababisha marudio ambapo Chakwera alishinda mwaka 2020.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!