Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

CHAN 2024:….HIVI NDIVYO TZ INAVYOWEKA NA KUVUNJA REKODI MPYA KILA MECHI….

  • 47
Scroll Down To Discover

LICHA ya kwamba haikuonyesha kiwango cha kutisha kulinganisha na ilivyocheza mechi ya ufunguzi wa fainali za CHAN 2024, lakini rekodi zimeandikwa na Taifa Stars imewapa kile ambacho Watanzania walio wengi wana hamu ya kukiona.

Stars ilipata ushindi wa pili mfululizo wa michuano ya CHAN 2024 ikiwa ni rekodi kwani haijawahi kutokea kwa timu hiyo kufanya hivyo katika fainali zote zilizowahi kufuzu barani Afrika kuanzia AFCON hadi hizo za CHAN.

Ilianza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso, kisha juzi usiku ikashinda kwa bao 1-0 mbele ya Mauritania na kufikisha pointi sita Kundi B, ikiwa haijawahi kufikisha pointi hizo katika fainali mbili za awali za mwaka 2009 na 2020 na hata zile za Afcon 1980, 2019 na 2023.

Katika mechi iliyokuwa na presha kwa timu zote mbili, beki wa Stars, Shomari Kapombe aligeuka shujaa baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Mauritania na kuiweka Tanzania hatua moja mbele kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Bao hilo pekee lilifungwa dakika za lala salama na kuibua shangwe za aina yake kutoka kwa zaidi ya mashabiki 14,000 waliojitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa, likihitimisha mechi hiyo iliyokuwa ya kuvutia kwa dakika zote 90.

NDOTO YACHANUA

Kwa ushindi huu wa pili mfululizo Kundi B, Tanzania sasa imefikisha pointi sita na ipo kileleni mwa kundi ikiwa haijaruhusu bao lolote, mafanikio yanayozidi kuongeza matumaini ya kuona Stars ikivuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mashindano haya kwa wachezaji wa ndani Afrika.

Fainali za mwaka huu ni za tatu kwa Tanzania kushiriki baada ya kufanya hivyo 2009 iliposhiriki katika kundi A na kuishia hatua ya makundi, ikimaliza nafasi ya tatu na pointi nne.

Baada ya hapo, Tanzania ikashiriki tena mwaka 2020 na kuishia tena makundi, ilipomaliza nafasi ya tatu kundi D na pointi nne, nyuma ya Guinea iliyoongoza na pointi tano sawa na Zambia iliyomaliza ya pili, huku Namibia ikiburuza mkia na pointi moja.

KIPINDI CHA KWANZA

Katika mchezo wa juzi pamoja na Tanzania kuwa nyumbani na kushinda mechi ya kwanza kwa 2-0 dhidi ya Burkina Faso, pambano dhidi ya Mauritania halikuwa rahisi hata kidogo.

Mauritania walikuja na ari ya kutafuta ushindi baada ya kutoka sare ya 0-0 dhidi ya Madagascar. Katika dakika 45 za kwanza, walionekana kumiliki mchezo kwa kipindi kirefu, wakicheza pasi za haraka na kutengeneza nafasi za hatari.

Wachezaji kama Mohamed Zweide, Ahmed El Moctar na El Mami Tetah walionyesha uelewano mkubwa, huku safu ya kiungo ya Tanzania ikionekana kuzidiwa nguvu nyakati fulani.

Hata hivyo, kipa Yakoub Suleiman aliibuka kuwa ngome muhimu kwa Tanzania, akiokoa mashuti mawili ya hatari katika dakika ya 17 na kabla ya mapumziko, akiokoa kombora la chini lililotoka kwa Moctar.

Tanzania, kwa upande mwingine walionekana kuwa na tahadhari zaidi kuliko kusuka mashambulizi, lakini ilikuwa ikipoteza mipira ovyo na kushindwa kutumia nafasi ilizotengeneza na kuwafanya mashabiki uwanjani kuishi kwa wasiwasi kwa dakika za pambano hilo kwa jumla.

KILICHOIBEBA STARS

Katika kipindi cha pili, Kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alifanya mabadiliko ya kimkakati, akiwaingiza Ahmed Pipino na Nassor Saadun wachezaji waliokuja na kasi na ubunifu.

Hapo ndipo mechi ilipoanza kufunguka. Tanzania iliongeza mashambulizi kwa kasi huku Mauritania wakionekana kuchoka kimwili. Pipino hata hivyo aliumia na kutolewa tena, nafasi yake ikichukuliwa na Shekhan Ibrahim aliosaidia kuifanya Stars irejee katika ubora katika kipindi hicho cha pili.

Mwishowe, jitihada zililipa katika dakika ya 88, baada ya kipindi kirefu cha Stars kushindwa kutumia nafasi ilizozitengeneza, alikuwa ni Kapombe ambaye aliwapa raha Watanzania.

Akiwa kwenye kasi na utulivu, Kapombe alipokea pasi ndefu ya juu kutoka kwa Idd Seleman ‘Nado’ na kupiga shuti kali ka kutumia mguu wa kushoto akiweka mpira upande wa kulia wa lango na kumfanya kipa Abderrahmane Sarr kushindwa la kufanya.

MSIKIE KAPOMBE

“Kusema kweli ilikuwa mechi ngumu sana. Tulijua kabisa Mauritania hawatakuja kutupa mchezo mwepesi. Walikuwa imara, walicheza vizuri, lakini tuliamini kwenye mipango ya kocha na tukapambana hadi mwisho,” alisema Kapombe.

Beki huyo aliongeza: “Nilipofunga lile bao, sikujua hata nifanye nini. Nilisikia tu kelele, nilikimbia tu. Kila mchezaji anatamani kufunga bao muhimu kwa taifa lake, nami nilipata nafasi hiyo leo (juzi). Ni jambo nitakalolikumbuka.”

“Kabla ya mechi, kocha alituambia nini cha kukifanyia kazi. Tuliambizana, tusifanye makosa madogo, tuwe watulivu, tusipaniki. Na tulifuata kila alichotuambia. Ushindi huu si wa mchezaji mmoja, ni wa timu nzima. Kila mmoja alitoa mchango wake,” alisema.

KITUO KINACHOFUATA

Kocha wa Madagascar, Romuald Rakotondrabe bado anaamini timu yake ina nafasi ya kushinda mechi ijayo na anatarajia upinzani mkubwa kutoka kwa Tanzania ambayo Jumamosi itakuwa ikitaka kujihakikishia kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

“Sare si mwisho wa dunia. Tulijifunza mengi. Tunakuja na mbinu mpya dhidi ya Tanzania na tunaamini tunaweza kushinda,” anasema.

Kocha huyo anaongeza: “Tunawaheshimu, siyo kuwaogopa. Tuna mpango wetu.”

Akiongelea mechi ijayo kocha Morocco anasema; “Tunajua bado kazi haijaisha. Madagascar ni timu nzuri, lakini kila mechi tunaingia kwa malengo mapya. Tutapambana kufanikisha kile ambacho kila Mtanzania anatamani kuona tukikifanya.”

The post CHAN 2024:….HIVI NDIVYO TZ INAVYOWEKA NA KUVUNJA REKODI MPYA KILA MECHI…. appeared first on Soka La Bongo.



Prev Post PAMOJA NA KUWA NO 5 KWA UBORA AFRIKA….CAF WAITUPA SIMBA LIGI YA ‘MCHANGANI’ ….
Next Post HUKO YANGA MAMBO NI 🔥🔥🔥🔥….BALAA LA HUYO CONTE NA ‘CASEMIRO’ LIGI IANZE TU….
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook