Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

TAASISI YA KIMATAIFA YA FISCH YATABIRI UIMARA UCHUMI WA TANZANIA

  • 9
Scroll Down To Discover

Taasisi ya Fitch imeendelea kuiweka Tanzania kwenye ukadiriaji wa B+ yenye Mtazamo Thabiti, hatua inayomaanisha kuwa nchi inaendelea kuonekana kuwa na uchumi unaokua na deni linaloweza kudhibitiwa, licha ya kuwepo kwa hatari kadhaa muhimu.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, “Mtazamo Thabiti” unaashiria kuwa Fitch haitarajii hali ya uchumi wa Tanzania kubadilika kwa kiwango kikubwa kuwa bora zaidi au mbaya zaidi katika muda mfupi ujao.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa nguvu, huku ukitarajiwa kufikia takriban asilimia 6 mwaka 2026 na 2027, kiwango kinachozidi nchi nyingi zilizo katika kundi hilo la ukadiriaji. Ukuaji huo unachangiwa na sekta za kilimo, madini pamoja na miradi ya miundombinu ikiwemo Standard Gauge Railway na East African Crude Oil Pipeline.
Aidha, mfumuko wa bei umeelezwa kuwa uko katika kiwango cha chini, hali inayotafsiriwa kuwa chanya kutokana na bei kutopanda kwa kasi kubwa.
Kwa upande wa fedha za serikali, Fitch imebainisha kuwa nakisi ya bajeti inatarajiwa kubaki katika kiwango cha wastani cha takriban asilimia 3 ya pato la taifa (GDP), huku deni la serikali likitarajiwa kupungua taratibu kutoka asilimia 50 hadi asilimia 47 katika miaka michache ijayo. Hali hiyo inaonesha kuwa nchi haikopi kupita kiasi.
Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa ukusanyaji wa mapato unaendelea kuboreka, jambo linaloashiria kuimarika kwa uwezo wa serikali kukusanya kodi. Vilevile, Tanzania inaendelea kunufaika na msaada chini ya programu ya IMF, hali inayoongeza imani kwa wawekezaji kuhusu mwendelezo wa mageuzi.
Hata hivyo, Fitch imeainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili nchi, ikiwemo kiwango cha chini cha ukusanyaji wa mapato ya serikali ikilinganishwa na nchi nyingine zenye hadhi sawa, hali inayofanya kuwa vigumu kufadhili huduma za umma na miradi ya maendeleo bila kutegemea mikopo au misaada ya nje.
Pia imeelezwa kuwa bado kuna wasiwasi kuhusu masuala ya utawala, uimara wa taasisi na ubora wa sera, mambo yanayoathiri mtazamo wa wawekezaji na wakopeshaji wa kimataifa.
Kwa upande mwingine, ripoti imeeleza kuwa akiba ya fedha za kigeni bado ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya nchi kulipia uagizaji na majukumu ya nje. Inatarajiwa kuwa akiba hiyo itafikia uwezo wa kufidia takriban miezi 2.5 ya malipo ya nje, kiwango kilicho chini ya wastani wa nchi zilizo na ukadiriaji kama huo.
Imebainishwa kuwa hali hiyo inaweza kuleta shinikizo endapo bei za bidhaa muhimu zinazoagizwa kama mafuta na mbolea zitapanda kwa kasi katika soko la dunia. Aidha, mgogoro wa muda mrefu unaohusisha Iran na eneo la Ghuba umetajwa kuwa unaweza kuongeza gharama za uagizaji, kupunguza watalii na kuongeza shinikizo kwenye akiba ya fedha za kigeni.
Kwa ujumla, Fitch imeeleza kuwa Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika maeneo ya ukuaji wa uchumi, udhibiti wa mfumuko wa bei, usimamizi wa deni na mwendelezo wa mageuzi, lakini bado inahitaji kuimarisha ukusanyaji wa mapato, utawala na uthabiti wa fedha za kigeni ili kuboresha zaidi hadhi yake ya ukadiriaji.



Prev Post CAG: DENI LA SERIKALI BADO NI HIMILIVU
Next Post TANZANIA HOLDS B+RATING AS ECONOMY SHOWS STRONG GROWTH
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook