Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Jica Yaahidi Kuendelea Kuishika Mkono Serikali Ya Tanzania – Majaliwa

  • 27
Scroll Down To Discover

▪JICA, Benki ya Dunia na AFDB watoa Dola za Marekani mil 516 miradi ya kilimo

▪Washauri elekezi wawili Mjapan na Mtanzaniia wawekwa TIC kurahisha uwekezaji

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) limeihakikishia Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa itaendelea kushirikiana nayo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.

Hatua hiyo imetokana na namna ambavyo Serikali imekuwa ikisimamia kikamilifu matumizi ya fedha mbalimbali zinazotolewa na wadau wa maendeleo likiwemo shirika hilo. Waziri Mkuu amesema “Serikali itaendelea itaendelea kusimamia ipasavyo fedha zote za maendeleo zinazoletwa nchini na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.”

Ameyasema hayo juzi (Jumatano, Mei 28, 2025) alipokutana na Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki Katsura kwenye ukumbi wa Mikutano wa Tachibana uliopo katika hotel ya New Otani, Tokyo nchini Japan akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa JICA kuendelea kutafuta wadau zaidi wa maendeleo kwa ajili upatikanaji wa fedha zitakazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwafanya Watanzania kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Amesema lengo la wito huo ni kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa wanafungua milango ya kiuchumi ili wananchi wengi washiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kujiongezea kipato.

“Lengo la kutafuta wadau hawa ni kuwawezesha wananchi washiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi, wanaotaka kuingia kwenye biashara, wanaotaka kuingia kwenye kilimo, sekta ya madini, sekta ya uvuvi na ufugaji haya ni maeneo ambayo tumeyawekea umuhimu.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona wananchi wanaendesha shughuli za kibiashara kukiwa na huduma zote katika mazingira rahisi, ikilinganishwa pia na utekelezaji wa miradi ya elimu, afya, miundombinu, nishati, ujenzi wa barabara pamoja na kilimo ni maeneo yanayotiliwa mkazo.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki Katsura alisema shirika lao linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali nchini kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo Benki ya Dunia katika mradi wa Ustahimilivu wa Chakula.

Makamu huyo wa Rais wa JICA alisema kuwa shirika lao litaendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini ikiwemo ya kuimarisha sekta ya miundombinu na usafirishaji.

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde ametumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa JICA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 516 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kilimo.

Mheshimiwa Silinde ametaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Ustahimilivu wa Chakula (TSRP) unaogharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 371 ambazo kati yake Benki ya Dunia imetoa Dola milioni 300.05 na JICA imetoa Dola milioni 71.09, ambapo utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030.

Amesema mradi mwingine ni wa Tanzania Agricultural Inputs Support Project (TAISP) unaotekelezwa kwa ubia kati ya Benki ya Maendeleo Afrika na JICA unaohusika na utoaji wa ruzuku katika pembejeo za kilimo.

Waziri Shilinde amesema mradi huo unaotarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 145, ambapo kati ya fedha hizo, JICA wanatoa dola milioni 70 na AfDB dola milioni 75.49 na ulianza kutekelezwa mwaka 2024 na utakamilika 2028. Tayari dola milioni 40 zimelipwa kwa kampuni 17 kwa ajili ya usambazaji wa mbolea.

Waziri Silinde amesema fedha hizo zimetolewa baada ya wadau hao kuridhishwa na namna ambavyo Serikali inasimamia sekta ya kilimo kwa mafanikio makubwa. Hata hivyo amewaomba wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan waje kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji hususan kwenye teknolojia ya umwagiliaji.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Ali Mohamed Ameir amesema katika vikao hivyo amewahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan uwepo wa mazingira wezeshi ya kutekeleza majukumu yao Zanzibar ikiwemo hali ya amani na utulivu.

Pia, Mheshimiwa Ameir ametumia fursa hiyo kuiomba JICA kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukamilisha miradi miwili ya ujenzi ikiwemo upanuzi wa soko na jiko la samaki katika eneo la Malindi hususani kutoa vifaa kwa wafanyabiashara pamoja na mradi wa usambazaji maji mijini katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Miradi yote inatekelezwa kwa awamu ya pili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri ameishukuru Serikali ya Japan kupitia JICA kwa kugharamia washauri elekezi wawili ambao watakuwa kiungo kati ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na Tanzania.

Amesema washauri hao elekezi ambao watakuwepo TIC mmoja ni Mtanzania na mwingine Mjapani watakuwa na majukumu ya kutoa taarifa za namna ya kufanikisha uwekezaji kati ya Tanzania na Japan.

“Lengo la huyu mwelekezi kutoka Japan ni kuzungumza na kusaidia makampuni na wawekezaji kutoka Japan kupata taarifa za namna ya kuja kuwekeza Tanzania na huyu wa Tanzania ni kusaidia Watanzania wote wanaotaka kuuza bidhaa zao Japan waweze kupata usaidizi kupitia kituo cha uwekezaji.”

Awali, Meneja Uenezi na Masoko wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Khamis Dunia alisema ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan umeiwezesha mamlaka yao kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo Zanzibar.

Alisema mbali na maonesho hayo, pia kitendo cha kushiriki katika mikutano iliyomhusisha Waziri Mkuu pamoja na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Kijapan vilivyofanyika jijini Tokyo alipata fursa ya kuelezea vipaumbe vya uwekezaji vilivyopo Zanzibar ikiwemo uchumi wa buluu na utalii jambo ambalo liliwavutia wawekezaji hao ambao tayari baadhi yao wameonesha nia ya kuwekeza Zanzibar.



Prev Post John Heche Aongoza Ziara ya Kumbukizi kwa Hayati Ndesamburo
Next Post CCM Yazindua Ilani ya Uchaguzi 2025–2030, Yataja Vipaumbele Tisa – (Picha +Video)
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook