

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhia rasmi hatua ya Tanzania kuanza maandalizi ya kuwa mwenyeji wa fainali za mashindano ya Unyange Duniani mwaka 2027, tukio kubwa la kimataifa linalotarajiwa kuleta mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali nchini.
Akizungumzia hatua hiyo mara baada ya kikao muhimu kilichofanyika hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema uamuzi huo ni mkakati wa kukuza vipaji, kuendeleza sekta ya sanaa, kuongeza mapato ya utalii na zaidi kutangaza chapa ya Tanzania kimataifa.

“Ukiondoa matukio ya awali yanayoambatana na shindano hili kwa muda wa mwaka mzima, fainali zake tu huhudhuriwa na takribani watu 5,000 ukumbini, na huangaliwa na watu zaidi ya bilioni moja duniani kote,” alifafanua Dkt. Abbasi.
Kwa mujibu wa maelezo yake, Tanzania inatarajia kunufaika na maelfu ya wageni kutoka mataifa mbalimbali, fursa za uwekezaji katika miundombinu ya burudani na utalii, pamoja na kutoa majukwaa ya kimataifa kwa wasanii na wabunifu wa ndani.
Fainali za Unyange Duniani (Miss World) ni moja ya matukio makubwa ya burudani na utamaduni yanayovuta hisia za watu duniani, huku yakihusisha washiriki kutoka mataifa zaidi ya 100, zikitangaza si tu uzuri wa nje bali pia maarifa, vipaji na mchango wa wanawake katika jamii.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!