

Dar es Salaam 8 Juni 2025: Mkurugenzi wa Msama Promotion na Muandaaji wa Tamasha la Msama Promotion, Alex Msama, ametoa tamko kali akiwataka wale wanaotukana na kuandika matusi mitandaoni kuacha mara moja. Katika mazungumzo yake na wanahabari mapema leo, amesema kuwa nchi yetu inakabiliwa na changamoto nyingi kuelekea uchaguzi mkuu, na ni muhimu kuheshimu mamlaka.

Msama alisisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameteuliwa na Mungu kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.
Aliongeza kuwa, kwa sasa Rais Samia anakaribia kumaliza kipindi chake, akitarajia kuingia kwenye awamu ya pili. Hivyo basi, ni muhimu kwa wananchi, hususan wale wanaojihusisha na dini, kumheshimu Rais na mamlaka zake.
“Baadhi ya watu wamekuwa wakiandika jumbe za matusi na kudharau mamlaka, jambo ambalo linapaswa kuacha mara moja.
Siasa hazipaswi kuchanganyikana na mambo ya ibada,” alisema Msama na kuonya kwamba miongoni mwa watumishi wa dini, kuna wale wanaojaribu kupeleka siasa ndani ya nyumba za ibada, hali inayohatarisha umoja na amani.
“Siasa si sehemu ya ibada, nyumba za ibada ni mahali pa kumuabudu Mungu, iwe ni kanisani au msikitini.
Ikiwa unataka kuzungumzia siasa, basi acha mambo ya dini na uelekee kwenye siasa ni muhimu kwa watumishi wa Mungu kuelewa majukumu yao na kujitenga na mambo yasiyofaa,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Msama, ni jukumu la kila mmoja wetu kuheshimu mamlaka na kuzingatia maadili ya kitaifa ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa na amani na maendeleo wakati huu wa kuelekea uchaguzi.
HABARI NA PICHA ZOTE: NEEMA ADRIAN WA GLOBAL PUBLISHERS
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!