
Waandishi wa habari kutoka Kanda ya kaskazini wameaswa kuzingatia sheria na maadili huku wakitanguliza uzalendo kwa Nchi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi hususani kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu 2025.
Wito huo umetolewa Agosti 16, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Salim Kalli wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya habari na utangazaji kuelekea Uchaguzi Mkuu ambao umewakutanisha Makamanda wa Polisi, Maafisa wa Polisi Jamii, Maafisa habari wa Jeshi la Polisi na Waandishi wa habari kutoka kanda ya Kaskazini inayojumuisha Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.
Mkuu huyo wa Wilaya ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema Waandishi wa habari ni watu muhimu sana katika jamii, hivyo wanaowajibu mkubwa wa kutoa taarifa za kweli na zenye usahihi zilizothibitishwa kutoka mamlaka husika.
Pia amewataka kutenda haki kwa kutoa habari bila kuwa na upendeleo ikiwa ni pamoja na kujiepusha na utoaji wa taarifa za uongo ambazo zitaleta chuki katika jamii katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu 2025.
Kwa upande wake Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime wakati akitoa mada katika mkutano huo, amesisitiza umuhimu wa Waandishi wa habari na Askari Polisi kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma zao kwa kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi na kuepuka upotoshaji unaoweza kuleta taharuki na wakati mwingine kusababisha uvunjifu wa amani katika jamii.
Kadhalika, DCP Misime amebainisha kuwa waandishi wa habari wanamchango mkubwa katika kulinda amani,utulivu na usalam katika jamii, hivyo ni vyema kuwa na ushirikiano mzuri na Jeshi la Polisi ili kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kulinda amani na utulivu wakati huu wa Uchaguzi mkuu.
Aidha, amebainisha kuwa Jeshi la Polisi limejipanga vyema kuhakikisha Uchaguzi Mkuu 2025 unafanyika kwa amani na utulivu kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine. Wakati wa kutekeleza majukumu yao watazingatia weledi na kufuata sheria sambamba na kutenda haki haki.
Mkutano huo wa siku moja umefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) ukiwa na lengo la kuwakumbusha wadau hao juu ya wajibu wao wa kuhakikisha taarifa zinazotolewa zinajenga taswira nzuri kwa jamii katika kulinda usalama wa nchi yetu.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!