
Historia nyingine imeandikwa jana jioni katika mji wa Kibaigwa, Dodoma, baada ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupokelewa kwa shamrashamra kubwa na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwa wingi.
Dkt. Samia alikuwa anatokea mkoani Morogoro, ambako alikuwa amehitimisha mkutano wake wa kampeni, na kuelekea mkoani Dodoma kuendeleza safari yake ya kuomba ridhaa ya kuongoza tena taifa.
Kwa mujibu wa mashuhuda, zaidi ya wananchi laki mbili (200,000) walijitokeza Kibaigwa wakiwa na nyimbo, nderemo, matarumbeta, zawadi na mabango yenye jumbe mbalimbali za kumuunga mkono, hali iliyoonesha upekee wa mapokezi hayo.
Wananchi walifurika barabarani kuanzia mapema mchana, huku wengine wakisubiri kwa masaa kadhaa ili kushuhudia msafara wa Dkt. Samia, ambaye aliwasili jioni na kulakiwa kwa shangwe kubwa.
Viongozi wa CCM mkoani Dodoma walisema tukio hilo ni uthibitisho wa mapenzi ya wananchi kwa Rais Samia, huku likiashiria mwamko wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Mama amepokelewa kwa heshima kubwa. Wananchi wameonesha wazi imani yao kwake na hamasa ya kuhakikisha safari ya maendeleo inaendelea,” alisema mmoja wa viongozi wa chama hicho mkoani humo.
Kwa upande wao, wananchi walioshiriki mapokezi hayo walisikika wakipaza sauti kwa kauli mbiu ya “Mama, jiandae kuongoza tena”, wakimaanisha kumuunga mkono Dkt. Samia kuendelea na muhula wa pili wa uongozi wake.
Kibaigwa, ikiwa kitovu cha biashara na kilimo katika mkoa wa Dodoma, kimekuwa kitovu cha kisiasa chenye mvuto mkubwa, na mapokezi hayo yameelezwa kuwa ni miongoni mwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mikutano ya kampeni nchini.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!