
Chama cha ACT Wazalendo kupitia Tawi la Mafifi, kata ya Kihesa mkoani Iringa, kimemvua rasmi uanachama wake Monalisa Joseph Ndala kwa madai ya kushindwa kutekeleza matakwa ya Katiba ya chama, hatua ambayo inahusishwa moja kwa moja na mvutano wa hivi karibuni kuhusu uteuzi wa mgombea urais wa chama hicho.
Kwa mujibu wa barua rasmi yenye kumbukumbu ya tarehe 28 Agosti 2025 iliyosainiwa na Katibu wa Tawi, Neema Ernest Kivamba, kikao cha tathmini cha Kamati ya Uongozi kilibaini Ndala amepoteza sifa za kuwa mwanachama hai chini ya Katiba ya ACT Wazalendo ya mwaka 2015 (toleo la 2024).
“Umepoteza sifa za kuwa Mwanachama halali na hai wa Chama cha ACT Wazalendo kwa mujibu wa Katiba ya ACT Wazalendo ya Mwaka 2015 Toleo la Mwaka 2024, Ibara ya 8(2)(a)(b), Ibara ya 13(1)(c)(d) pamoja na Ibara ya 97(b)(d),” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Uamuzi huo umeambatana na kufutwa kwa kadi ya uanachama wa Ndala pamoja na kuondolewa jina lake katika regista ya wanachama wa Tawi la Mafifi.
Mvutano wa Uteuzi
Hatua hiyo imeibuka siku chache tu baada ya Ndala kupinga uhalali wa mchakato wa uteuzi wa Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea urais wa ACT Wazalendo. Ndala alidai kuwa uteuzi huo ulikiuka kanuni kwa kuwa Mpina alijiunga na chama tarehe 5 Agosti 2025, nje ya muda wa kurejesha fomu.
Pingamizi hilo lilipelekea Msajili wa Vyama vya Siasa kutengua uteuzi wa Mpina, akieleza kulikuwa na dosari za kikatiba na kikanuni, hatua iliyozua mtikisiko mkubwa ndani ya chama.
ACT Yapeleka Kesi Mahakamani
Baada ya maamuzi hayo, ACT Wazalendo iliwasilisha kesi Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumuondoa Mpina kwenye orodha ya wagombea. Chama kimeeleza kuwa INEC haina mamlaka ya kumuengua mgombea kwa maelekezo ya Msajili.
Katika uamuzi wake wa hivi karibuni, Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia Masijala Kuu Dodoma imeipa Serikali muda wa siku tano pekee kujibu kesi hiyo, baada ya kukataa ombi la upande wa Serikali la kuongezewa siku 14.
ACT Wazalendo na Mpina wanadai kuwa INEC ilikiuka Katiba, Sheria na Kanuni za Uchaguzi wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea Urais uliofanyika Agosti 27, 2025.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!