

Juba, Sudan Kusini – Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kufunguliwa mashtaka mazito dhidi ya Makamu wa Rais wa Kwanza, Riek Machar, ikimtuhumu kwa ugaidi, uhaini, mauaji na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Hatua hii, iliyotangazwa rasmi na Wizara ya Sheria siku ya Alhamisi, Septemba 11, imeibua hofu kubwa ya kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Kulingana na taarifa ya serikali, Machar na washitakiwa wenzake saba wanadaiwa kuhusika na shambulio la kijeshi lililofanyika kaskazini mwa nchi mwezi Machi. Shambulio hilo liliua zaidi ya wanajeshi 250, akiwemo meja jenerali wa jeshi la Sudan Kusini na rubani wa Umoja wa Mataifa. Baada ya tukio hilo, Machar alikamatwa na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani, ambako amekuwa kwa zaidi ya miezi sita sasa.
Historia ya mvutano
Machar, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mpinzani mkuu wa Rais Salva Kiir, amejikuta mara nyingi katikati ya siasa zenye mgawanyiko wa kikabila na mapigano ya silaha. Baada ya taifa hilo jipya kujinyakulia uhuru mwaka 2011, mvutano kati ya wawili hao ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa takriban miaka minne, vikiua mamia ya maelfu na kuwahamisha mamilioni ya raia.
Chini ya shinikizo la kimataifa, Kiir na Machar walilazimika kukubali mpango wa kugawana madaraka kupitia serikali ya mpito. Hata hivyo, mahusiano yao yameendelea kudorora, na mapigano ya hivi karibuni pamoja na kukamatwa kwa washirika wa karibu wa Machar yameonyesha wazi namna tofauti zao bado ni kubwa.
Hofu ya kurudi kwa vita
Mashitaka haya mapya yanahofiwa kuwa kichocheo kipya cha vurugu na mapigano ya kisiasa, huku jamii ya kimataifa ikitoa tahadhari. Wachambuzi wanasema hatua hiyo inaweza kuvuruga makubaliano ya amani ya 2018 na kusababisha taifa changa zaidi duniani kuingia tena katika mzunguko wa umwagaji damu.
Kwa sasa, Machar na wenzake wanatarajiwa kufikishwa mahakamani, ingawa wachambuzi wanaonya kuwa mchakato huu wa kisheria unaweza kugeuka jukwaa la kisiasa na kuongeza mgawanyiko badala ya kuleta maridhiano.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!