
Hatima ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, inatarajiwa kujulikana Jumatatu, Septemba 15, 2025, saa 3:00 asubuhi, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam.
Uamuzi huo utatolewa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Ndunguru, baada ya kumaliza kusikiliza hoja za pande zote mbili kufuatia mapingamizi yaliyowekwa na Lissu, ambaye katika shauri hilo anajitetea mwenyewe.
Kwa siku nne mfululizo kuanzia Jumatatu ya Septemba 8, 2025, Mahakama ilisikiliza hoja hizo ambapo Lissu aliomba kesi hiyo ifutwe akidai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyosikiliza hatua za awali za shauri hilo haikuwa na mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
Iwapo Mahakama Kuu itakubaliana na hoja za Lissu, kesi hiyo inaweza kufutwa rasmi. Hata hivyo, kama hoja hizo zitakataliwa, kesi itaendelea kusikilizwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!