MABOSI wa Yanga wakishirikiana na benchi la ufundi la klabu hiyo, wameanza kupiga hesabu la kufyeka mastaa sita wa timu hiyo, wakiwamo wazawa watano na mmoja wa kigeni, huku kiungo mshambuliaji, Clatous Chama ikielezwa amewagawa mabosi hao juu ya uamuzi wa kumtema au kumbakisha kikosini.
Yanga iliyoweka rekodi ya aina yake msimu wa 2024-2025 kwa kubeba jumla ya mataji matano, ikiwamo kutetea Kombe la Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) kwa msimu wa nne mfululizo sambamba na Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano na lile la kimataifa la Toyota, imeanza mipango kwa kusuka kikosi kipya cha msimu ujao.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, zimedokeza kuwa, kwa sasa mabosi wa Yanga wapo bize kupitia ripoti ya kocha Miloud Hamdi kuhusu wachezaji wanaostahili kufyekwa, ukiacha wale waliomaliza mikataba yao akiwamo Kennedy Musonda inayeelezwa hatakuwapo kwa msimu ujao.
Inaelezwa, majina ya walio katika hatari ya kufyeka ni watano wazawa, akiwamo Jonas Mkude ambaye inaelezwa kama ilivyo kwa Chama kwa nyota wa kigeni bado jina lake linajadiliwa kama asalie kwa msimu ujao au aingie kwenye panga hilo litakalohusisha pia nafasi ya kipa na eneo la ushambuliaji.
“Tunahitaji kukiboresha zaidi kikosi chetu, tuna timu nzuri lakini tunahitaji kuiongezea nguvu zaidi, wapo wachezaji ambao wanamaliza mikataba kama unavyojua, msimu umemalizika, wapo ambao tutawapa nafasi ya kuendelea kwa kuwaongezea mikataba,” alisema mmoja wa mabosi wa klabu hiyo kongwe iliyotwaa mataji zaidi ya 50 tangu mwaka 1965, yakiwamo 31 ya Ligi Kuu, aliyeongeza;
“Wapo wanaomaliza mikataba na kwa namna walivyotumika katika msimu unaona kabisa wameshindwa kuongeza ushindani dhidi ya wenzao hawa tutawaruhusu kutafuta nafasi sehemu nyingine.
“Kuna wengine tutaachana nao kutokana na viwango, lakini hapa nazungumzia kundi la wachezaji wa kigeni nako tutafanya tathmini, akili yetu hapa ni kuwa na kikosi bora zaidi ya hiki cha msimu uliokwisha.”
Mwanaspoti linafahamu, wapo mastaa ambao wataondoka kwa sababu ya mikataba na wengine viwango vyao ambavyo havijawaridhisha mabosi hao, lakini idadi ya waliopendekezwa ni wazawa watano na kigeni mmoja, japo Musonda inaelezwa tayari ameshajua hatma yake nje ya kundi hilo.
Hata hivyo, hadi sasa majina kamili ya wazawa watano walio hatarini kupitiwa na panga hilo ili kupisha sura mpya kuingia kikosini, huku majina ya kina Feisal Salum, Gibril Sillah, Josephat Bada na wengine yakitajwa miongoni mwa silaha mpya ya Yanga za msimu ujao, japo haijathibitishwa rasmi.
CHAMA NA MKUDE
Miongoni mwa mastaa ambao wamefanikiwa kubeba ubingwa wakiwa Simba na Yanga ni pamoja na Clatous Chama na Jonas Mkude ambao wote wanamaliza mikataba yao msimu huu.
Lakini kwa upande wa Mzambia huyo alionekana katika paredi la ubingwa akiwa na vaibu zuri na mabosi wa klabu hiyo akiwamo Rais wa klabu hiyo Hersi Said, inaelezwa amewaga mabosi wa Yanga.
Hapo awali inadaiwa kuwa, kilichokwamisha kiungo huyo kusaini hadi sasa ni dau ambalo Yanga imeliweka kutomridhisha Chama.
Huku katika timu yake ya zamani Simba ikigoma kumweka katika hesabu za msimu ujao, kwa sababu ya namna alivyoondoka.
Msimbazi pia wanahofia nafasi ya Charles Ahoua ambaye ameuwasha sana msimu huu, akimaliza kama kinara wa mabao wa klabu na msimu kwa ujumla akifunga 16.
Chama ambaye hakupata nafasi ya kucheza muda mrefu ndani ya Yanga amemaliza msimu akiwa na amefunga mabao sita.
The post WANAOPIGWA PANGA YANGA HAWA HAPA….JINA LA CHAMA LAWEKEWA ‘FAILI’ MAALUMU…. appeared first on Soka La Bongo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!