Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Mbatia Ashinda Kesi Dhidi ya NCCR Mageuzi, Uongozi Wake Watambuliwa Tena na Mahakama

  • 25
Scroll Down To Discover

Aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia ameshinda kesi aliyoifungua dhidi ya chama hicho, akipinga kuondolewa kwenye uongozi na kuvuliwa uanachama wake.

Mbatia aliemnguliwa madarakani kufuatia mkutano mkuu wa NCCR Mageuzi uliofanyika Septemba 24, 2022, ambapo pia ulimvua uanacama, jambo alilopinga katika shauri la madai nambari 18/2023 (Judicial Review) alilofungua Mbatia dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya chama hicho.

Akitoa hukumu hiyo leo Mei 28, 2025, Jaji Jaji A. Kagomba wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu Dodoma, ametengua uamuzi wote wa Mkutano Mkuu wa NCCR-Mageuzi wa Septemba 24, 2022 uliopindua uongozi wa Mbatia na kukubaliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo Jaji Kagomba amesema hoja ya kwamba, Ndugu James Mbatia hakuwa mwanachama wa Chama cha NCCR-Mageuzi kwa sababu kadi yake ni ya mwaka 1992 wakati usajili kamili ni wa mwaka 1993; haina mantiki yoyote kwa sababu mwaka 1992 ilikuwa ni usajili wa muda wa vyama vya siasa na ndio wanachama hao waliowezesha chama kupata usajili wa kudumu hata Katiba ya NCCR-Mageuzi ni ya mwaka 1992.

Kuhusu uamuzi ya mkutano Mkuu wa Septemba 24, 2022 Jaji amesema haukumpatia haki ya msingi (Natural Justice) Mbatia ya kusikilizwa hivyo ulikiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya chama cha NCCR-Mageuzi na sheria za vyama vya siasa.

Pia, Jaji ametengua maamuzi yote yaliyofanywa na Mkutano huo ya kumuondolea Ndugu Mbatia uanachama na Uenyekiti wa Chama, akikitaka pia chama hicho kulipa gharama zote za kesi.

Akizungumzia hukumu hiyo, Mbatia amesema ataanza kuchukua hatua mapema kuitekeleza.

“Hiyo ni judicial review (mapitio ya mahakama) haina haja ya kusubiri wakate rufaa, kwa hiyo nitachukua hatua mapema,” amesema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Joseph Selasini aliyesema kuwa ameiona hukumu hiyo, amesema kwa maoni yake Mahakama haijamrejeshea uenyekiti Mbatia, bali inataka apewe muda wa kujitetea.
“Kwa mujibu wa hukumu ile, Mbatia hakupewa nafasi ya kujitetea katika mkutano mkuu, maana yake ni kwamba ni lazima uitishwe mkutano mkuu ili aitwe ajitete. Haimaanishi kwamba Mahakama imetengua uamuzi wa mkutano mkuu uliofanyika pale Jeshi la Wokovu (Dar es Salaam),” amesema.

Amesema uamuzi wa kukata rufaa utafikiwa na vikao vitaka’vyotafakari hukumu hiyo.



Prev Post “WAKATI UNAPOHISI HOFU ZAIDI, NDIO WAKATI WA KUFANIKIWA” ALISEMA BABU HUYO…!
Next Post Rais Samia: CCM Kufanya Mikutano kwa Njia ya Mtandao kwa Mujibu wa Kanuni
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook