Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Waziri Mkuu Majaliwa Azindua Mradi wa Maji Hungumalwa Wilayani Kwimba

  • 34
Scroll Down To Discover

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na ujenzi wa miradi ya maji katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo karibu na makazi yao.

Ameyasema hayo Jumapili, Mei 18, 2025 wakati akizungumza na wananchi katika Eneo la Hungumalwa wilayani Kwimba, Mwanza baada ya kuzindua mradi wa maji Hungumalwa akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza. Mradi huo wa maji wa Hungumalwa ulianza kutekelezwa tarehe Machi 08, 2022 na ulikamilika Agosti 15, 2024.

Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza wananchi kuendelea kuiamini na kushirikiana na Serikali ambayo imedhamiria kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao. Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ya elimu, maji, afya na ujenzi wa barabara.

”Tutaendelea kusimamia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na tutaendelea kutekeleza ilani kwa vitendo. Kwenye elimu tunaendelea kukarabati na kuimarisha shule zote za msingi na sekondari. Tutawahudumia wananchi wala msiwe na mashaka. Suala la maji tunaendelea kuhakikisha yanapatikana maeneo yote.”

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mwanza, Mhandisi Godfrey Sanga amesema gharama ya mkataba ni shilingi bilioni 11, ambapo mpaka sasa kazi zote zimekamilika kwa thamani ya shilingi bilioni 10 na kufanya salio katika mkataba wa ujenzi wa mradi huo kuwa ni shilingi milioni 201.

Meneja huyo ametaja kazi zilizopangwa kufanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa tangi moja lenye ujazo wa lita milioni moja, ununuzi wa mabomba na viungio vyake km 54.817, uchimbaji na ufukiaji mitaro yenye urefu wa km 54.817, kuunganisha maji kwa wateja wa majumbani 500, ujenzi wa ofisi ya chombo cha watumia maji ngazi ya jamii na ujenzi wa nyumba ya mlinzi, ambapo kazi zote zimekamilika.



Prev Post Profesa Janabi Ashinda Nafasi ya Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika
Next Post Boni Yai: Mbowe Hana Uhusiano na Wanaojiondoa Chadema – Video
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook