

Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) limetangaza kuandaa maandamano ya amani nchi nzima, ikiwa ni ishara ya kulaani na kukemea kitendo cha kushambuliwa kwa wakili Deogratius Mahinyila na askari wa Jeshi la Polisi, Septemba 15, 2025, katika viwanja vya Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam.
Taarifa ya TLS iliyotolewa Septemba 18, 2025 na kusainiwa na Rais wa chama hicho, Boniface Mwabukusi, imeeleza kuwa maandamano hayo yatashirikisha mawakili wote nchini na yataambatana na tamko maalum litakalosomwa na viongozi wa TLS katika kila mkoa.
“TLS kupitia Baraza la Uongozi, ipange na kutangaza siku rasmi ya maandamano ya amani ya mawakili wote nchi nzima kama ishara ya kulaani kitendo alichofanyiwa Wakili Deo Mahinyila pamoja na mawakili wengine waliowahi kupitia udhalilishwaji, manyanyaso au uonevu wakati wakitekeleza majukumu yao,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
TLS imesisitiza kuwa maandamano hayo yatalenga kulinda haki, utu na heshima ya kila wakili, ikionya kuwa shambulio kwa wakili mmoja ni shambulio kwa taaluma nzima ya sheria na ustawi wa haki nchini.
Hatua za Haraka
Mbali na maandamano, TLS imetangaza hatua nyingine za dharura, ikiwemo:
Kusitisha ushiriki wa mawakili katika kesi za msaada wa kisheria za jinai (Criminal Sessions Cases) na shughuli zinazohusisha Mahakama na Serikali.
Kufungua mashauri dhidi ya askari waliohusika kumshambulia Mahinyila.
Kumpa msaada wa kisheria Mahinyila katika kufungua mashauri hayo.
TLS pia imeelekeza kuwa mawakili wasipokee kesi za msaada wa kisheria hadi pale hatua za kisheria zitakapochukuliwa na taarifa rasmi kutolewa kuhusu askari waliohusika.
Wito kwa Serikali
Chama hicho kimeitaka Serikali, Mahakama na Jeshi la Polisi kutoa tamko rasmi na kuchukua hatua za haraka za kisheria dhidi ya waliomshambulia wakili huyo, kikiwaonya kwamba haki na heshima ya wanasheria nchini lazima ilindwe kwa gharama yoyote.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!