KIPYENGA kwa ajili ya kuanza kwa mashindano yaliyopo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ngazi ya klabu kimepulizwa tangu Jumanne wiki hii na Côte d’Or ya Seychelles ilipoteza nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya Stade d’Abidjan ya Ivory Coast, huku Foresters Mont Fleuri nayo ya Seychelles, ikipoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya FC 15 De Agosto ya Equatorial Guinea katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa wawakilishi wa Tanzania, kazi inaanza leo Ijumaa na Yanga ipo Angola kwa ajili ya mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao Wiliete, mchezo utakaopigwa kuanzia saa 12:00 jioni kwa saa za Tanzania.
Dimba la 11 de Novembro lililopo Talatona jijini Luanda, Angola lenye uwezo wa kuingiza watazamaji 48,500, ndilo litatumika kwa mchezo huo.
Ni mchezo ambao Yanga inakwenda kucheza ikiwa ni siku mbili zimepita tangu itoke kupambana na Simba katika Dabi ya Kariakoo na kushinda bao 1-0 kwenye Ngao ya Jamii.
Katika mchezo huo, Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine, alisema: “Wapinzani wetu ni mabingwa wa Angola, huwezi kuwa bingwa kwa bahati mbaya kwa sababu ligi ni safari ndefu, siyo mbio za muda mfupi, benchi letu la ufundi limefanya tathmini ya kina juu ya kikosi chao na tunatakiwa kupambana ili kufikia malengo yetu.
“Kama siku zote nimekuwa nikisema, niwaombe mashabiki watuombee dua njema na kwa hakika tutapata matokeo mazuri.”
Yanga iliyoanza safari kutoka Dar es Salaam juzi Jumatano saa 7 usiku kupitia Ethiopia, ilifika Angola siku hiyo hiyo saa 8 mchana, ilipata muda wa kupumzika, kabla ya kufanya mazoezi ya kuuweka mwili sawa.
Jana Alhamisi, kikosi hicho kilikuwa na programu mbili za maandalizi ya mchezo huo wa leo mbali na mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jioni kwenye uwanja wa mechi, pia benchi la ufundi lilikuwa na wasaa wa kupitia mikanda ya video.
Wakati Yanga ikiwa na jukumu la kupitia mikanda ya video kuwasoma zaidi wapinzani wao, kuna wachezaji watatu ambao wanatazamwa kama ndiyo wa kuchungwa zaidi, ukiachana na Skudu Makudubela ambaye aliwahi kuitumikia Yanga.
Wachezaji hao watatu wote walikuwepo katika mashindano ya CHAN 2024 ambao ni kipa Agostinho Calunga, kiungo Beni Jetour na mshambuliaji João Chingando Manha maarufu Kaporal.
Safu ya ulinzi ya Yanga inapaswa kumuangalia zaidi Kaporal ambaye katika michuano ya CHAN 2024, licha ya Angola kutotoboa hatua ya makundi, lakini alionyesha uwezo mkubwa wa kufunga kwenye mchezo dhidi ya Zambia akitikisa nyavu mara mbili.
HESABU MAKUNDI
Yanga kwa sasa hesabu zao ni kucheza hatua ya makundi ambayo msimu wa 2023-2024 ilirejea baada ya kupita takribani miaka 25. Kocha aliyefanya kazi hiyo alikuwa Miguel Gamondi. Msimu huo safari yao iliishia robo fainali. Kisha msimu uliopita 2024-2025 chini ya Gamondi, Yanga ikafuzu tena makundi ya michuano hiyo, hata hivyo hakuiongoza katika hatua hiyo, mkataba wake ukasitishwa na Sead Ramovic akachukua mikoba, timu ikaishia hapohapo makundi.
Ujio wa Romain Folz, unamfanya kocha huyo raia wa Ufaransa kuwa na kazi ya kuhakikisha Yanga inacheza tena hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo kama ambavyo uongozi wa klabu hiyo ulivyoweka malengo.
Kipindi cha usajili wa dirisha kubwa kilipofunguliwa Julai Mosi mwaka huu na kufungwa Septemba 7, 2025, Rais wa Yanga, Hersi Said, alinukuliwa akisema: “Usajili wa msimu huu utakuwa bora kuliko sajili ambazo tumewahi kuzifanya miaka ya hivi karibuni, pamoja na kubeba mataji yote lakini bado tuna deni kubwa kwa wana Yanga kubeba tena mataji yetu na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
“Tusidanganye, mashindano ya kimataifa yanahitaji uwekezaji mkubwa na uzoefu, tulicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilikuwa uzoefu wa mwaka mmoja, lakini kuna baadhi ya wachezaji wakaondoka, msimu uliofuata tukacheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu uliopita tuliishia makundi, huku kunahitaji uzoefu wakati huohuo kuna hitaji mwendelezo kwa hiyo mimi naweka tu malengo ya makundi.”
REKODI YA YANGA DHIDI YA WAANGOLA
Katika mashindano ya CAF, Yanga imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya timu za Angola kwani imezitoa mara mbili na mara ya kwanza kucheza dhidi ya timu za nchini huko ni mwaka 2007 dhidi ya Petro De Luanda kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali.
Mchezo wa kwanza ugenini, Yanga ilipoteza kwa mabao 2-0, lakini nyumbani ikashinda 3-0. Ikasonga mbele kwa matokeo ya jumla 3-2.
Baada ya hapo, mwaka 2016 Yanga ikacheza dhidi ya G.D. Sagrada Esperança katika Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya awali. Mchezo wa kwanza nyumbani Yanga ilishinda kwa mabao 2-0, ugenini ikapoteza kwa bao 1-0 lakini ikavuka kwa matokeo ya jumla 2-1.
CHUKUA HII
Kutoka mwaka 2007 hadi 2025, Yanga imekuwa ikicheza dhidi ya timu za Angola kila baada ya miaka tisa, huku ugenini ikipoteza na kushinda nyumbani. Ilikuwa 2007, 2026 na sasa 2025.
MECHI ZINGINE ZA LEO
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mbali na mchezo huo kati ya Wiliete dhidi ya Yanga, kuna zingine zinapigwa leo ambazo ni Dadjè ya Benin dhidi ya Al Ahli Tripoli kutoka Libya. Aigles du Congo ya DR Congo dhidi ya Rivers United kutoka Nigeria na African Stars ya Namibia dhidi ya Vipers ya Uganda.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, mechi za leo Ijumaa ni ASN Nigelec ya Niger vs Olympic Safi (Morocco), Aigle Royal (Cameroon) vs San Pédro (Ivory Coast) na Wolaitta Dicha (Ethiopia) vs Al Ittihad Tripoli (Libya).
The post KWA HALI HII…YANGA WANAKAZI YA KUFANYA ANGOLA LEO…WAKIKAA VIBAYA TU CHALII…. appeared first on Soka La Bongo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!