RATIBA ya Ligi Kuu Bara 025-2026 imetoka ambapo pazia litafunguliwa kesho, Septemba 17, 2025 kwa KMC kuikaribisha Dodoma Jiji saa 10:00 jioni huku Coastal Union ikipambana na Tanzania Prisons saa 1:00 usiku.
Hizi hapa timu zitakazokuwa na mechi nyingi saa 8:00 mchana zikiwemo Mashujaa, Tanzabia Prisons, KMC, Mbeya City, Pamba Jiji, Tabora United, Namungo na Singida Black Stars.
MASHUJAA FC
Mashujaa kwa ratiba ya awali inaonyesha ndiyo itakayokuwa na mechi sita za saa 8:00 mchana ikiwa ni idadi sawa na Tanzania Prisons pamoja na KMC.
Mechi ya kwanza ya Mashujaa itakuwa ugenini dhidi ya Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida, Septemba 30, kisha itafunga safari hadi jijini Mwanza kupambana na Pamba Jiji, Oktoba 17.
Baada ya hapo, itarejea Lake Tanganyika, Kigoma kuikaribisha Namungo, Oktoba 25, kisha itasubiri hadi Februari 2 kucheza mechi mbili ugenini na KMC na kuifuata Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Machi 4. Mechi ya sita itakayopigwa saa 8 itapigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, ambapo itakuwa na kibarua dhidi ya Tabora United, Machi 18, 2026.
TANZANIA PRISONS
Prisons itakuwa na mechi sita pia za saa 8:00 mchana, ikianzia ugenini Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora kupambana na Tabora United Novemba 22, kisha itarejea nyumbani kucheza dhidi ya Pamba Jiji, Desemba 3.
Mechi nyingine ni za nyumbani dhidi ya Coastal Union Februari 10 na Azam Februari 23, kisha dhidi ya KMC jijini Dar es Salaam Machi 12, 2026 na kuhitimisha na Dodoma Jiji Mei 2, 2026.
KMC
KMC itaanza mechi za mchana mwakani 2026, Uwanja wa KMC Complex kupambana na Mashujaa Februari 2, kisha kuifuata Singida Black Stars mjini Singida Machi 5.
Baada ya hapo, itaikaribiTanzania Prisons Machi 12, kisha itaifuata Mbeya City jijini Mbeya Machi 15, huku mechi inayofuata itakuwa na JKT Tanzania Aprili 6 na kurejea nyumbani kuikaribisha Coastal Union Mei 6, 2026.
MBEYA CITY
Timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu itacheza mechi tano za mchana ikianza na Fountain Gate ugenini Septemba 18, kisha kurudi nyumbani kucheza na Namungo, Novemba 28.
Baada ya hapo itacheza na Singida Black Stars, Desemba 4 kisha kuikaribisha KMC Machi 15, huku mechi ya mwisho ya saa 8 mchana kwa itasalia jijini Mbeya kupambana na Coastal Union Aprili 10.
PAMBA JIJI
Pamba itaanza kucheza mechi mbili za saa 8 jijini Mwanza Septemba 28 kwa kuikaribisha Tabora United na Mashujaa Oktoba 17, kisha itaifuata Tanzania Prisons, Desemba 3. Mechi mbili zitakazohitimisha tano za saa 8, itacheza zote nyumbani Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na Coastal Union, Februari 6, huku ya mwisho na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam, Februari 19, 2026.
TABORA UNITED
Kikosi hiki cha ‘Nyuki wa Tabora’, kitakuwa na mechi tano za saa 8, ambapo kitapambana na Pamba Jiji ugenini, Septemba 28, kisha kitarudi nyumbani kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora kucheza na Tanzania Prisons, Novemba 22, 2025.
Baada ya hapo, Tabora itasafiri hadi Manungu Complex kucheza na Mtibwa Sugar, Novemba 29, ikifuatiwa na Mashujaa ugenini Machi 18, 2026 na kuhitimisha mechi za saa 8 nyumbani mbele ya Fountain Gate Aprili 18, 2026.
COASTAL UNION
Timu hii itakuwa na kibarua cha kucheza mechi zote tano za saa 8 mchana ikiwa ugenini, ikianza na Pamba Jiji, Februari 6, 2026, TZ Prisons, Februari 10, 2026, Fountain Gate Machi 17, 2026, Mbeya City, Aprili 10, 2026 na KMC FC Mei 6, 2026.
SINGIDA BLACK STARS
Kikosi hiki kinachonolewa na Kocha, Miguel Gamondi, kitakuwa na mechi nne za saa 8 mchana, ambapo kitaanzia nyumbani kwa kupambana na Mashujaa Septemba 30, kisha baada ya hapo kitaenda hadi jijini Mbeya kucheza na Mbeya City Desemba 4, 2025.
Baada ya hapo, itakuwa na mechi mbili nyumbani, ikipambana na KMC Machi 5, 2026, huku ikihitimisha kwa kucheza na Mtibwa Sugar, Aprili 5, 2026, ikitazamiwa kuleta ushindani kutokana na mastaa waliopo, wakiwemo, Clatous Chama na Khalid Aucho.
MTIBWA SUGAR
Mtibwa iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025-2026, baada ya kushuka daraja msimu wa 2023-2024, itakuwa na mechi nne za mchana, ambapo tatu ni za nyumbani, ikianza na Tabora United, Novemba 29, 2025, kisha Namungo, Februari 7, 2026. Mechi nyingine ya nyumbani itakayocheza kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, itakuwa dhidi ya maafande wa kikosi cha Mashujaa Machi 4, 2026, huku moja iliyobakia itasafiri hadi Singida kupambana na Singida Black Stars, Aprili 5, 2026.
FOUNTAIN GATE
Timu hii itakuwa na mechi tatu za mchana kwa mujibu wa ratiba ya awali ya Ligi Kuu Bara, ambapo mbili zitakuwa nyumbani ikianza na Mbeya City, Septemba 18, 2025, Coastal Union, Machi 17, 2026, huku ya ugenini ni na Tabora United, Aprili 18, 2026.
NAMUNGO
‘Wauaji wa Kusini’, watakuwa na mechi tatu za mchana ambazo zote kikosi hicho zitakuwa za ugenini, ikianza na Mashujaa Oktoba 25, 2025, Mbeya City Novemba 28, 2025, kisha kuhitimishwa kwa kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar, Februari 7, 2026.
AZAM FC
Kikosi hichi cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam, kitakuwa na mechi mbili za mchana ambazo zote kitacheza kikiwa ugenini, ikianza na Pamba Jiji Februari 19, 2026, kisha baada ya hapo kitapambana na Tanzania Prisons Februari 23, 2026.
JKT TZ
Timu hii ya maafande, haitoathirika kutokana na Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo inaoutumia kuruhusiwa kuchezwa mechi za usiku hivyo, kikosi hicho kitacheza mchana dhidi ya KMC tu uwanjani hapo, pambano litakalopigwa rasmi Aprili 6, 2026.
DODOMA JIJI
Dodoma Jiji inayojulikana kama ‘Walima Zabibu’, itakuwa na mechi moja tu itakayochezwa mchana kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ambapo itasafiri kupambana na kikosi cha maafande wa Tanzania Prisons, pambano litakalopigwa Mei 2, 2026.
MSIKIE MAYANGA
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Salum Mayanga ambaye kikosi hicho kitakuwa na mechi sita za mchana, anasema licha ya ratiba hiyo ila anachokiamini sio suala la kucheza mapema, isipokuwa jambo muhimu la kuzingatia ni maandalizi mazuri ya wachezaji.
“Sio mara ya kwanza kwetu kucheza muda huo hivyo, hatuwezi kuona kama ni kitu kipya pia, ninachokiamini ni kuandaa vyema wachezaji kiakili na kimwili kutokana na mpinzani tutakayekutana naye, hilo ndilo ninaloweza kulisema,” anasema Mayanga.
The post LIGI KUU BARA 25/26….HIZI HAPA KUPIGWA WAKATI JUA LA UTOSI 🌞🌞…. appeared first on Soka La Bongo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!