

Autaja mradi wa barabara kutoka Ruangwa hadi Nachingwea na Mradi wa maji Nyangao-Ruangwa hadi Nachingwea
Asema anamfahamu Liwaka kwa uchapakazi wake
Liwaka asema Rais Dkt. Samia ni kiongozi mwenye uthubutu na maamuzi
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 13, 2025 amezindua kampeni za Ubunge jimbo la Nachingwea zilizofanyika katika uwanja wa maegesho ya Malori Nachingwea mjini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuchagua wagombea wote wa chama cha mapinduzi ifikapo Oktoba 29 mwaka huu ili waendee kuitekeleza ilani uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030 na kuiwezesha Nachingwea kuendelea kupaa kwa kasi kimaendeleo.
“Jitokezeni kwa wingi kwenda kupiga kura ifikapo oktoba 29, nendeni mkamchague Rais Dkt. Samia kwa kura nyingi, kamchagueni pia Fadhili Liwaka hatupaswi kulala, hata kama ni mgombea pekee nendeni mkaweke tiki muda utakapofika”

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Wilaya za Ruangwa na Nachingwea zimeendelea kunufaika na miradi ya maendeleo ikiwemo mradi mkubwa wa maji kutoka Nyangao, Ruangwa hadi Nachingwea ambao unaendelea kutekelezwa. “Mradi huu utakaonufaisha vijiji vya Ruangwa ma Nachingwea utagharimu shilingi bilioni 119”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa tayari Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nachingwea.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa amefanya kazi kwa karibu na Liwaka kwa kipindi kirefu, na anamfahamu kwa uchapakazi wake na anaamini atajitoa kwa ajili ya maendeleo ya wananachingwea. Ninamfahamu Liwaka, anajua namna ya kuchapa kazi”
Kwa upande wake, mgombea ubunge jimbo la Nachingwea Fadhili Liwaka amesema kuwa katika kipindi chake atajielekeza katika sekta za kimaendeleo ikiwemo Miundombinu, Elimu, Afya, Kilimo na Ufugaji.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu moja ya kiu yangu kubwa katika sekta ya miundombinu ni ujenzi wa barabara ya Nachingwea hadi Masasi kwa kiwango cha lami, pamoja na hili, elimu ni agenda kubwa niliyonayo ninataka kupunguza idadi ya wanafunzi hasa wa kike wanaolala nyumbani na kwenda shuleni asubuhi kwa kujenga mabweni”.
Pia, Liwaka amesema kuwa moja ya ndoto yake kubwa aliyonayo ni kuhakikisha anamaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji. “Mheshimiwa Waziri Mkuu ninatamani siku moja tufanye sherehe wafugaji walete ng’ombe tuchinje na wakulima walete mahindi tupike tusherehekee”.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!