
Doha, Qatar – Watu sita wamepoteza maisha katika shambulio la anga la Israel lililolenga viongozi wa Hamas waliokuwa kwenye kikao mjini Doha, huku kundi hilo likidai viongozi wake wakuu wamenusurika.
Hamas imesema shambulio hilo lililenga timu yake ya mazungumzo iliyokuwa ikijadili pendekezo jipya la Marekani la kusitisha mapigano Gaza. Licha ya uharibifu mkubwa uliosababishwa, kundi hilo limesisitiza kuwa jaribio la Israel la kuua viongozi wake limefeli.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametetea hatua hiyo akisema shambulio hilo lilikuwa “halali kabisa,” kwa kuwa liliwalenga wapanga mashambulio ya Oktoba 7, 2023, ambayo yalianzisha vita vya Gaza.
Rais wa Marekani, Donald Trump, hakuficha kutoridhishwa kwake. “Sijafurahishwa… sijaridhishwa na hali hii. Sio nzuri kabisa,” alisema, akiongeza kuwa lengo kuu linabaki ni kurudishwa kwa mateka walioko mikononi mwa Hamas.
Serikali ya Qatar, ambayo imekuwa mpatanishi muhimu kati ya Israel na Hamas, imelilaani shambulio hilo na kulitaja kama “uoga” na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Qatar pia ni mwenyeji wa ofisi ya kisiasa ya Hamas tangu mwaka 2012 na ni mshirika mkuu wa Marekani katika eneo hilo.
Mashambulio haya yameibua taharuki kubwa ya kidiplomasia, yakionekana kusogeza mbele vita vya Gaza kuvuka mipaka, na kuifanya Doha – kituo kikuu cha mazungumzo ya amani – kuwa uwanja mpya wa mzozo wa Mashariki ya Kati.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!