- Amy Walker, Philippa Roxby & Rozina Sini
- BBC
Idadi ya watoto waliozaliwa Uingereza na Wales, kwa sasa iko chini zaidi tangu miaka ya 1970, takwimu rasmi zinaonyesha.
Kiwango cha uzazi - hutazama ni watoto wangapi wanaozaliwa na kila mwanamke wakati wa miaka yake ya kuzaa – kwa sasa kiko chini zaidi katika rekodi.
Uingereza sio nchi pekee yenye tatizo hilo - nchi nyingi zinakabiliwa na kupungua kwa uzazi na zingine zinafanya juhudi kubwa kuongeza uzazi.
Nini kimesababisha kuanguka kwa uzazi? Kuna gharama kubwa ya kulea watoto, kufanya kazi na changamoto ya kupata mpenzi sahihi.
Lakini pia kuna ushahidi kwamba vijana wengi hawana mpango wa kuwa na watoto kabisa – nje ya sababu hizo.
BBC imezungumza na wanawake wawili na wanaume wawili wenye umri wa miaka thelathini - umri wa wastani ambapo kwa watu wa Uingereza na Wales wanakuwa wazazi - kupata mawazo yao juu ya suala hilo.
Kari, 34: Bora kuasili mtoto

Kari Aaron Clark, mtafiti katika Chuo cha Uhandisi cha Royal, anapata pauni 53,000 kwa mwaka lakini anahisi hawezi kumudu kulea mtoto huko London.
Miaka minne iliyopita, mshahara wake ulikuwa pauni 22,000 wakati akimaliza PhD yake.
Mpenzi wake Kaitlyn, ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa PhD, ana matatizo sawa ya kifedha.
Ina maana licha ya mshahara wa juu kwa wastani wa Kari, amepata wakati mgumu kuweka akiba kwa ajili ya nyumba - jambo ambalo anaamini ni muhimu kabla ya kuwa mzazi kwa sababu ya hali ya "kutokuwepo kwa uhakika" katika kukodi.
Pia anataja gharama za malezi ya watoto. Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya shirika la hisani la watoto Coram, wastani wa gharama ya kila wiki ya kupata mlezi wa muda wote kwa watoto chini ya miaka mitatu nchini Uingereza ni pauni 300, ikilinganishwa na karibu pauni 430 katikati mwa London.
Kari anasema, Kaitlyn ana maoni kama yake na wote wana wasiwasi kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi.
"Napendelea sana wazo la kuasili mtoto. Kwa njia hiyo ninamsaidia mtu ambaye tayari anahangaika," anasema.
"Ninaweza kuasili mtoto baada ya kupitia hatua ya malezi ya utotoni."
Licha ya kukata tamaa kwa sasa juu ya uwezekano wa kuwa mzazi kibaolojia, Kari anasema "haondoshi uwezekano wa kuzaa moja kwa moja."
Chris na Jemma 33: Kufunga kizazi

Derevam Chris Taylor na mkufunzi wa mbwa Jemma Wrathmell kwa pamoja wanapata mapato ya pauni 60,000 na wamekuwa pamoja kwa miaka 11.
Wanandoa hao, wanaoishi Wakefield huko West Yorkshire, wanasema: "Tulikuwa na mazungumzo ya kina kujadili mambo kama shule, gharama na malezi," anasema Gemma.
Lakini hitimisho lilikuwa; gharama ni kubwa sana.
"Baada ya malipo ya bili zetu zote na mambo muhimu hakuna nafasi ya bajeti ya kumudu mtoto," anasema Chris.
Kwa sababu hiyo, wamechukua uamuzi - Chris anatarajia kufunga uzazi, baada ya miaka mingi ya Gemma kuzuia mimba.
“Baadhi ya watu wamesema utabadili mawazo, lakini wajue ni uamuzi wetu,” anasema Jemma.
Ellie, 39: Nimegandisha mayai
Ellie Lambert, anayeishi Sheffield, anataka kupata watoto lakini anasema hajapata mwenza anayefaa.
Miaka miwili iliyopita, alitumia pauni 18,000 kwa mizunguko miwili ya kugandisha yai. "Nachanganyikwa, ni gharama kubwa kwa kitu ambacho kinaweza kisisababisha chochote," anasema.
Anatarajia kuzitumia akikutana na mtu sahihi, au akifikia hali ya kifedha ambapo anaweza kuishi mwenyewe kwa usaidizi wa mtoaji mbegu.
Ellie anasema ana wasiwasi kuhusu gharama ya kifedha kwa mzazi mmoja.
Ripoti kutoka Child Poverty Action Group ya mwaka jana iligundua wastani wa gharama ya kulea mtoto hadi umri wa miaka 18 ni pauni 166,000 kwa wanandoa na pauni 220,000 kwa mzazi mmoja.
Ingawa Ellie alidhani angekutana na mtu kufikia mwishoni wa umri wa miaka 20, "licha ya kuwa kwenye programu zote za kutafuta mpenzi, bado hajafanikiwa."
Akiwa tayari ametumia akiba yake kugandisha mayai, anasema itamugharimu pauni 10,000 zaidi kutumia mbegu ili kupandikiza.
Dami, 34: Hadi niwe tayari

Kwa Dami Olonisakin, mwendesha kipindi cha ngono na uhusiano anayeishi London, maboresho ya matibabu ya uzazi - kama vile kugandisha yai - "yanawapa wanawake "nafasi zaidi kuliko hapo awali."
Kuwa mama, anasema, si jambo la "kulichukulia kirahisi."
"Gharama za malezi ya watoto zinapanda, sera za uzazi zina kikomo, kimsingi wanawake wanapaswa kufikiria sana," anasema.
Anasema hana haraka. "Sijisikii niko katika haraka ya kutulia na kupata watoto kwa sababu tu watu wanatarajia hilo," anasema.
Badala yake anaangazia kazi yake baada ya kukulia katika kaya ambayo "haikuwa na chochote".
"[Wazazi wangu] walijitahidi sana, lakini siku zote nimekuwa nikisema sitakuwa na mtoto hadi niwe tayari."
Hali ya baadaye
Haya yote yanaibua swali la kipi kitatokea siku zijazo - ikiwa watoto wachache ndio watazaliwa.
Kupungua kwa viwango vya uzazi haliwahusu tu watu kuchelewa kuzaa, lakini pia mwenendo unaokua wa watu kutotaka kuzaa kabisa, anasema Brienna Perelli-Harris, profesa wa demografia katika Chuo Kikuu cha Southampton.
Takwimu kutoka Utafiti wa hivi karibuni wa Uzazi na Jinsia nchini Uingereza, zinaonyesha watu wazima wasio na watoto hawana uhakika wa kupata watoto, huku robo ya wale wenye miaka 18 hadi 25 wakisema hawana uhakika au hawatakuwa na mtoto.
"Gen Z wana uwezekano mkubwa wa kutaka kuishi bila mtoto," anasema. "Hapo awali, lilikuwa jambo la ajabu - sasa linakubalika zaidi.
"Na hilo linatokana na mambo ya kiuchumi kama mapato, gharama za malezi ya watoto na ajira."
"Baada ya muda mrefu, idadi ya watu itaanza kupungua," anasema Prof Perelli-Harris.
Hivi ndivyo hali ilivyo nchini Uingereza na nchi zingine kama Uhispania na Italia, ambapo kiwango cha uzazi ni cha chini.
"Uhamiaji unaweza kuzuia kupungua kwa idadi ya watu au hata kubadili hali mambo," anasema Prof Perelli-Harris.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!