
KIEV, Ukraine – Ukraine imekataa pendekezo la Rais wa Urusi, Vladimir Putin, la kwamba Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, aende Moscow kwa ajili ya mkutano wa pamoja.
Taarifa hiyo imetolewa mapema leo, Alhamisi Septemba 4, 2025, na mtandao wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ujerumani (DW). Putin amesema kwamba awali alikuwa amejadili suala hilo na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu mkutano wake wa kilele na Trump mjini Alaska, akiwa nchini China, Putin alisema:
“Donald aliniuliza kama inawezekana kuandaa mkutano wa aina hiyo, nikamjibu ‘ndiyo, hilo linawezekana. Zelensky anaweza kuja Moscow ikiwa yupo tayari.'”
Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa X, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, ameweka bayana kuwa takribani nchi saba zimejitolea kuwa wenyeji wa mkutano kati ya Putin na Zelensky. Sybiha aliongeza kuwa Rais Zelensky yuko tayari kusafiri mara moja kwenda katika mojawapo ya nchi hizo kwa ajili ya mazungumzo, lakini sio kwenda Urusi.
Hali hii inaashiria mgogoro unaoendelea katika uhusiano wa pande mbili na kuonyesha hali ngumu ya diplomasia ya Ukraine na Urusi, licha ya shinikizo la kimataifa la kuanzisha mazungumzo ya amani.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!