
BOTI mpya ya kifahari (yacht) yenye thamani ya Dola za Kimarekani 940,000 (sawa na takribani Shilingi Bilioni 2.3 za Kitanzania) imezama dakika 15 pekee baada ya kuzinduliwa rasmi majini, tukio lililoacha wengi midomo wazi.
Ajali hiyo imetokea takribani mita 200 kutoka ufukweni katika wilaya ya Eregli, mkoa wa Zonguldak, kaskazini mwa Uturuki, siku ya Jumanne.
Mashuhuda walisema yacht hiyo ilianza kupoteza mlingano mara tu baada ya kushushwa majini, na hatimaye kuzama kwa haraka. Mmiliki wa meli hiyo, ambaye alikuwemo ndani, alilazimika kuogelea mwenyewe kuelekea ufukweni. Hakuna taarifa za majeruhi wengine zilizoripotiwa.
Tukio hili limezua mjadala mkali mitandaoni, wengi wakishangazwa na jinsi chombo cha kifahari chenye thamani kubwa kiasi hicho kilivyoshindwa kudumu hata robo saa baharini. Wengine wameeleza masikitiko yao kwa hasara kubwa iliyompata mmiliki, huku baadhi wakigeuza tukio hilo kuwa utani mitandaoni.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!