Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Dkt. Mpango Atoa Wito kwa Waganga Wakuu Kuhamasisha Afya Bora kwa Wananchi

  • 38
Scroll Down To Discover

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuongeza juhudi katika kutoa hamasa kwa wananchi ili kuzingatia kanuni za afya bora na kuchukua hatua madhubuti za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Amesema ni vema elimu itakayotolewa izingatie ujenzi na matumizi ya vyoo bora, unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni nyakati zote muhimu ili kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza, uondoshaji salama wa majitaka katika ngazi ya kaya na maeneo ya umma pamoja na kutibu maji ya kunywa kwa njia ya kuchemsha au kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa rai kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuvitunza vifaa tiba ikiwemo mashine za kisasa za uchunguzi na matibabu pamoja na magari ya kubeba wagonjwa yaliyonunuliwa na Serikali ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kutoa huduma kwa watu wengi zaidi.

Pia amewasihi kuimarisha eneo la utunzaji wa kumbukumbu za matumizi ya dawa na vifaa tiba ili kuleta ufanisi katika utunzaji wa dawa na vifaa tiba na kuepuka upotevu. Amesema kutokuwepo na kumbukumbu sahihi za matumizi ya dawa na vifaa tiba hutatiza katika usambazaji wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa, na kutoa mwanya wa wizi na matumizi yasiyo sahihi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kulipa kipaumbele suala la utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya dawa ili kuisaidia jamii kutambua na kuepuka madhara ya matumizi holela ya dawa hususani dawa za maumivu na antibiotics ambazo zikitumiwa kiholela madhara yake ni makubwa. Pia amewataka kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa kiapo cha maadili katika kuwahakikishia wananchi huduma bora.

Mkutano huo wa siku tatu una kauli mbiu isemayo “Wajibu wa Waganga Wakuu wa Miko ana Halmashauri katika kuimarisha Ubora wa Huduma za Afya kuelekea Bima ya Afya kwa Wote”



Prev Post Kuwa sehemu ya bilioni 1.5 kutoka LOOT Legends, Ni Meridianbet Pekee
Next Post PITIA VICHWA VYA HABARI KATIKA MAGAZETI YA LEO JULAI 13, 2025
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook