
Serikali ya Iran imetoa takwimu mpya za vifo vilivyosababishwa na vita vya hivi karibuni dhidi ya Israel, ikisema kuwa angalau watu 1,060 wamepoteza maisha. Onyo limetolewa kwamba idadi hiyo huenda ikaongezeka na kufikia 1,100, kutokana na majeraha mabaya yaliyowakumba baadhi ya waathirika.
Takwimu hizo zilitolewa na Saeed Ohadi, mkuu wa Foundation of Martyrs and Veterans Affairs, katika mahojiano yaliyorushwa na televisheni ya taifa ya Iran usiku wa kuamkia Jumanne.
Katika siku 12 za mashambulizi makali ya anga kutoka Israel, Iran ilijaribu kupunguza ukubwa wa hasara iliyopata. Hata hivyo, baada ya kutangazwa kwa kusitishwa kwa mapigano, Tehran imeanza kukiri kiwango kikubwa cha uharibifu ulioikumba nchi hiyo — zikiwemo ngome muhimu za kijeshi, mifumo ya ulinzi wa anga, na sehemu za miundombinu ya nyuklia.
Mpaka sasa, Iran haijatoa taarifa kamili kuhusu kiwango cha vifaa vya kijeshi ilivyopoteza, lakini mashirika huru yanaendelea kutoa takwimu mbadala. Shirika huru lenye makao yake mjini Washington, Human Rights Activists, limesema kuwa watu 1,190 waliuawa, wakiwemo 436 raia wa kawaida na 435 wanajeshi au maafisa wa usalama. Kulingana na shirika hilo, watu wengine 4,475 walijeruhiwa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!