
Chama cha ACT Wazalendo kimepinga vikali hatua ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumzuia mgombea wao wa Urais, Luhaga Joelson Mpina, kurejesha fomu za uteuzi, kikieleza kuwa maamuzi hayo kuwa si tu ya aibu, bali yanaibua maswali mengi juu ya Uadilifu, Umakini, weledi na uhuru wa Tume ambayo imepewa dhamana.
Kwenye barua yao, ACT Wazalendo imeeleza namna ilivyoshangazwa na maelekezo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi kupitia barua ya tarehe 26 Agosti 2025, kwamba Mpina asifike Ofisi za Tume kwa ajili ya uteuzi kwa kisingizio cha kupokea nakala ya barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa iliyotengua uteuzi wake.
“Tunaiomba sana Tume iepuke mtego wa kuifanya itekeleze majukumu yake kinyume na mipaka ya kisheria na katiba na kuwa chanzo cha kusigina misingi ya haki, Demokrasi na utawala bora.
“Tunaiomba Tume itengue barua ya Mkurugenzi wa Uchaguzi yenye Kumb. Na. CBA. CEA.75/162/24/4 ya tarehe 26 Agosti, 2025 kwa Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo na kuruhusu Ndugu Luhaga Joelson Mpina, Mgombea wa Kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT Wazalendo kurudisha fomu kama alivyopangiwa awali kupitia barua ya Tume yenye Kumb.Na. CBA.75/165/01A/229 ya tarehe 15 Agosti, 2025”__imeeleza barua ya ACT Wazalendo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!