
Dar es Salaam, Agosti 26, 2025 – Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeomba kwa dharura kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili kuwasilisha maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu changamoto zinazohitaji kutatuliwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, alisema chama hicho tayari kimewasiliana rasmi na Ofisi ya Rais kwa lengo la kufikisha maazimio na mapendekezo yaliyotolewa na wadau mbalimbali wa siasa na demokrasia nchini.
“TLS imewasiliana na Ofisi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwasilisha maazimio ya wadau. Lengo ni kutoa ushauri wa hatua za haraka kuchukuliwa ili kurudisha imani ya wananchi na kuhakikisha uchaguzi unakuwa shirikishi, shindani na wenye uhalali wa kisiasa,” alisema Mwabukusi.
Amesisitiza kuwa, licha ya kutuma maombi hayo, mpaka sasa bado hawajapata majibu kutoka Ikulu, lakini wanaendelea kusisitiza umuhimu wa mazungumzo hayo kufanyika mapema ili taifa liingie kwenye uchaguzi likiwa na mshikamano wa kitaifa.
Mwabukusi aliongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha misingi ya haki na demokrasia nchini:
“Tunayo nafasi ya kusimama imara kama taifa kwa kusikilizana na kuelewana kwenye masuala muhimu ya kitaifa, kama suala la uchaguzi mkuu,” alisema.
TLS imekuwa ikihimiza mjadala wa kitaifa na mashirikiano kati ya wadau wote wa kisiasa, kijamii na kisheria ili kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru, wa haki na wenye kuakisi misingi ya kidemokrasia.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!