

Kutoka kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu Mei 19.2025 kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Wakili Tundu Lissu ililetwa kwa ajili ya kutajwa, ambapo upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika
Jamhuri imesema mpaka sana shauri hilo linaendelea na uchunguzi chini ya mamlaka za Kipolisi, na kwamba kwakuwa upelelezi haujakamilika hivyo wanaiomba Mahakama kuhairisha kesi husika kwa siku 14 zaidi, jambo ambalo limeonekana kupingwa vikali na Mawakili wa utetezi
Jopo la Mawakili wa utetezi likiongozwa na Mawakili waandamizi Mpale Mpoki, Dkt. Rugemeleza Nshala na Peter waliwasilisha maombi kadhaa Mahakamani hapo, ambapo miongoni mwake wameiomba Mahakama ‘kulazimisha’ upande wa Jamhuri ueleze nini hasa kinachokwamisha upelelezi kwa sababu mwanzo ilidaiwa Mahakamani hapo kuwa ushahidi wote kuhusiana na shauri hilo upo mtandaoni
Jambo la pili walilowasilisha Mawakili wa utetezi Mahakamani hapo ni kwamba, hawafurahishwi namna ambavyo mteja wao anavyokuwa amezungukwa na maafisa wa Jeshi la Magereza (askari), ambapo wameishawishi Mahakama kutoa amri ya kuwaondoa askari wote ‘wanaomlinda’ Lissu ndani ya chumba cha Mahakama, kwakuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 Mahakama haimtambui mtuhumiwa kama ‘mkosaji’ na kwamba kitendo cha mteja wao kuzungukwa na askari wengi haikubaliki
Ukijibu hoja hizo, upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa licha ya kwamba Katiba imeeleza hivyo, lakini haijatoa maelekezo ya aina gani ya ulinzi inahitajika kwa mtuhumiwa pindi anapokuwa ndani ya chumba cha Mahakama, hivyo kuiomba Mahakama kutupilia mbali maombi hayo na kwamba ikiwezekana wanaomba ulinzi huo uongezwe
Mawakili hao wa serikali wameenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa suala la ulinzi lina faida kwa mtuhumiwa mwenyewe, Mahakama na maafisa wa Mahakama kwa ujumla wake.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!