
Faraja Nyalandu Kotta, aliyewahi kuwa mrembo wa taji la Miss Tanzania mwaka 2004, si jina geni katika tasnia ya urembo nchini. Hata hivyo, nyuma ya tabasamu lake la kuvutia na taji la heshima, kuna hadithi ya mwanamke jasiri, mama, mjasiriamali na kiongozi wa mabadiliko katika elimu kupitia teknolojia.
“Nilipopewa taji la Miss Tanzania nilianza kujiona mtu mwenye wajibu kwa jamii,” anasema Faraja kwa sauti ya utulivu lakini iliyojaa msisitizo.
Kupitia nafasi yake hiyo, alisafiri sehemu mbalimbali, kushiriki katika shughuli za kijamii, na kufanya kazi na taasisi mbalimbali – uzoefu uliomfungulia macho na moyo juu ya changamoto zinazowakabili Watanzania wengi, hasa katika sekta ya elimu.
Kutoka kwenye Urembo hadi Sheria na Teknolojia
Baada ya Miss Tanzania, Faraja aliendelea na masomo ya shahada ya Sheria nchini Uingereza. Wakati huo, akiwa mama, mwenye watoto wawili na mke, changamoto zilikuwa kubwa.
“Ilikuwa kazi kubwa sana kusoma nikiwa na familia. Nilijifunza kufanya yote kwa kutumia teknolojia,” anakumbuka kwa hisia.
Ndipo alipoanza kuona nguvu ya teknolojia katika kuboresha maisha, hasa kwa wanawake na wazazi wanaotafuta elimu. Alipoamua kurudi Tanzania baada ya masomo, alikuta taifa likiwa katika wimbi la kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi wa sekondari.
“Niliona kuna uhitaji mkubwa wa kusaidia wanafunzi na walimu kupata vifaa vya kujifunzia kwa njia ya teknolojia,” anasema.
Hapo ndipo wazo la Shule Direct lilipochipuka mwaka 2013 – jukwaa la kidijitali linalotoa maudhui ya kielimu moja kwa moja kwa wanafunzi na walimu kupitia mtandao.
“Shule Direct ni kama darasa mkononi – unapata vitabu, maswali, na maelezo moja kwa moja, bila kulazimika kuwa darasani,” anaeleza.
Wakati wazo hilo likianza, teknolojia ilikuwa bado changa na wengi hawakulielewa. Lakini leo, Shule Direct inatumika na mamilioni ya wanafunzi na walimu kote nchini. Kupitia jukwaa hilo, wanafunzi wanapakua maudhui ya kujifunzia, huku walimu wakipata vifaa na maarfa ya kufundishia.
Mwaka 2018, Shule Direct ilianza kutumia teknolojia ya akili bandia (AI) kupitia mfumo uitwao Teacher Kidevu, ambao huandaa na kusambaza maudhui ya elimu kwa njia bunifu. Mfumo huo sasa ni sehemu rasmi ya jukwaa la Shule Direct.
Kwa sasa Mtandao wa Shule Direct umekuwa na watumiaji takribani milioni tano na imepakuliwa na watu zaidi ya laki tatu.
Kuzaliwa kwa NdotoHub
Pamoja na hili la elimu, Faraja pia ni mwanzilishi wa NdotoHub, mradi unaolenga kuwawezesha wasichana na wanawake vijana katika ujasiriamali na ubunifu. Faraja anasema NdotoHub ni sawa na mtoto wa ShuleDirect.
“Ninataka kusaidia wasichana kutimiza ndoto zao. Kama ninaweza kuwa sehemu ya mafanikio yao hata kwa asilimia moja, nitakufa nikiwa na furaha,” anasema kwa kujiamini.
Kupitia NdotoHub, mafunzo, mitaji na ushauri hutolewa kwa wanawake wajasiriamali na wanaoanzisha mashirika au kampuni.
Lengo ni kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi na wajasiriamali wanaojitegemea.
Kutambuliwa Duniani
Juhudi zake hazikupita kimya. Mwaka 2020, World Economic Forum ilimtambua Faraja kama mwanamke anayeongoza mabadiliko kupitia teknolojia. APP ya Shule Direct imepakuliwa zaidi ya mara 2000, na matumizi yake yanaongezeka kila siku.
Kwa Faraja, mafanikio haya ni mwanzo tu.
‘Naamini kila mtu ana uwezo wa kufanikiwa, tunahitaji maarifa na elimu bora ili kila mtu atimize ndoto zake”anamalizia Faraja.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!