
Kitamaduni Mapapa huchaguliwa na makasisi wakuu wanaoitwa Makadinali kupitia mchakato wa uchaguzi wa siri ulioanzia karne nyingi nyuma.
Papa mpya huchaguliwa baada ya aliye madarakani kufariki, au baada ya kujiuzulu (kama Papa Benedict XVI alivyofanya, mwaka 2013).
Mrithi wake anakuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki la Roma – Papa Mkuu. Pia makadinali ndio wanaomchagua Papa mpya.
Kuna makadinali 252 kote ulimwenguni kufikia tarehe 19 Februari 2025, ambao kwa kawaida pia ni maaskofu. Na wale walio chini ya umri wa miaka 80 ndio wanaostahili kumpigia kura papa mpya.
Idadi ya makadinali wanaopiga kura kwa kawaida hupunguzwa hadi 120, lakini kwa sasa kuna 138 kati yao ambao wana vigezo vya kushiriki katika kumchagua Papa mpya. (Papa Francis aliteua Makadinali wapya 21 mwezi Desemba 2024.)
Ukifika muda wa kumchagua Papa mpya, Makadinali wote wanaitwa Vatikani Roma kwa mkutano. Kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi ambao umefanyika kwa karibu miaka 800.
Katika siku ya kwanza ya kongamano hilo, wanafanya Misa (ibada la Kikristo) katika Kanisa la St Peter’s Basilica. Kisha wanakusanyika katika Kanisa la Sistine la Vatikani. Huko, agizo la extra omnes hutolewa. Ni lugha ya Kilatini ikiwa na maana “kila mmoja atoke nje.”
Kuanzia wakati huo, Makadinali wote watawekwa ndani ya Vatican hadi papa mpya atakapochaguliwa.
Makadinali wanaopiga kura wana chaguo la kuanza kupiga siku ya kwanza wakiwa Sistine Chapel. Kuanzia siku ya pili na kuendelea, hupiga kura mara mbili kila asubuhi, na mara mbili kila alasiri, hadi mgombeaji wa upapa apatikane mmoja.
Katika kura hizo, kila Kadinali anayepigakura huandika jina la mgombea anayempendelea kwenye karatasi za kupigia kura. Ili kuficha kura, Makadinali wanaambiwa wasitumie mtindo wao wa kawaida wa mwandiko.
Hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya kampeni za wazi. Vatican inasema makadinali wanaongozwa na Roho Mtakatifu.
Mara mbili kila siku, karatasi za kupigia kura zilizotumika huchomwa moto. Na watu walio nje ya Vatikani wanaweza kuona moshi ukitoka kwenye bomba la kanisa la Sistine Chapel.
Rangi nyeusi au nyeupe huwekwa kwenye karatasi hizo. Karatasi hizo zikichomwa hutoa moshi kulingana na rangi iliyochomwa. Moshi mweusi unaashiria bado hakuna matokeo; moshi mweupe unaonyesha kuwa Papa mpya amechaguliwa.
Na Elvan Stambuli, GPL.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!