

Taarifa hiyo imetolewa na ZANZIBAR-Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani Halali wa Biashara (ZFCC) wamepiga marufuku uingizaji wa bidhaa za chakula kwa watoto maarufu kama chama ambazo zimeambatanishwa na zawadi hatarishi, kutokana na kuanza kusababisha madhara kwa watoto watumiaji.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kusambaa kwa picha jongofu inayoonesha kisa cha mtoto kumeza zawadi hizo na kupata madhara ya kiafya upande wa Tanzania bara na baadhi ya taarifa zinazoeleza kushawishika kula kupita kiasi kutokana na mvuto wa zawadi zinazowekwa ndani ya vifungashio vya bidhaa hiyo.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika katika ofisi za ZFDA Mombasa, Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Usalama wa Chakula, Dkt. Khamis Omar alisema, lengo la mkutano huo ni kujadili usalama wa watoto dhidi ya athari zinazotokana na zawadi hizo, na kuweka miongozo madhubuti ya kudhibiti hali hiyo bila kuathiri watumiaji na wafanyabiashara.
“Tumeamua kuchukua hatua mapema kabla tatizo halijawa kubwa. Tayari kuna taharuki kuhusu matumizi ya zawadi hizi hata kama baadhi ya matukio hayajatokea rasmi Zanzibar. Hatutaki kusubiri madhara ndipo tuchukue hatua,” alisema Dk. Omar.
Alisema, bidhaa zenyewe (chama) zimeonekana kuwa salama, lakini zawadi zinazoambatanishwa nazo hasa zile ndogo au zinazofanana na chakula zimekuwa chanzo cha hatari, kwani watoto wamekuwa wakizimeza kimakosa.
Pia aliwaasa wazazi na walezi kuwa makini na bidhaa hizo wakati mamlaka zikiendelea na udhibiti, akibainisha kuwa usalama wa mtoto ni jukumu la pamoja.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ZFCC, Aliyah Emanuel Juma, aliwaonya wafanyabiashara dhidi ya kutumia zawadi hizo kama mbinu za kibiashara zinazolenga kuvutia watoto na kuwalaghai wazazi.
“Kutoa zawadi si kosa, lakini inapokuwa zawadi hiyo ni hatari au haijapimwa ubora wake, basi tunahatarisha maisha ya wateja wetu, hasa watoto. Tunahitaji maadili na uadilifu katika biashara,” alisema Aliyah.
Kwa mujibu wa sheria ya Tume ya Ushindani Halali wa Biashara namba 5 ya mwaka 2018, kifungu cha 56 hadi 64, ni kosa kuingiza au kuuza bidhaa hatarishi zinazosababisha taharuki, akibainisha kuwa miongozo hiyo inalenga kulinda usalama wa mtumiaji.
Naye Mkaguzi wa Chakula kutoka ZFDA, Aisha Suleiman Mubandakazi, aliwataka wafanyabiashara wote kuhakikisha bidhaa zao zimesajiliwa rasmi ili ziweze kufanyiwa tathmini na kuhakikiwa kwa usalama wake.
“Wengi hawasajili bidhaa zao, hasa chama, na hivyo hushindwa kufanyiwa tathmini ya kitaalamu. Hii ni hatari kubwa kwa afya ya watoto wetu,” alisema Aisha.
Aliongeza kuwa, bidhaa zinazolenga watoto hupaswa kupitia mchakato maalum wa usajili kwa kuwa kinga ya miili yao ni dhaifu, hivyo huathirika haraka na sumu au vihatarishi vilivyomo kwenye chakula au zawadi.
Alisisitiza kuwa ZFDA haitasita kuchukua hatua kali kwa wafanyabiashara wanaokiuka sheria na miongozo ya uingizaji bidhaa, akiwataka waweke mbele maslahi ya afya za watumiaji badala ya faida.
Wakati huo huo, baadhi ya wazazi na wananchi walieleza wasiwasi wao na kupongeza hatua hiyo ya serikali wakiomba kuwepo kwa kampeni za uelimishaji kwa wazazi kuhusu madhara ya zawadi hizo na kuhimiza udhibiti mkali wa bidhaa zote zinazoambatana na zawadi hatarishi.
“Watoto hawawezi kutofautisha kati ya chakula na vitu vya kuchezea. Tumeanza kuona watoto wakimeza zawadi bila kujua. ZFDA ifanye ukaguzi mkali,” alisema Salum Hassan, mzazi.
Nao wafanyabiashara waliunga mkono marufuku hiyo, ingawa walikiri kuwa itawapa changamoto kibiashara kwa kuwa soko la bidhaa hizo lilikuwa kubwa kutokana na zawadi.
“Ni changamoto lakini tunakubali. Afya ya mtumiaji ni muhimu zaidi. Tunaomba ZFDA ielekeze aina ya zawadi zinazokubalika ili tuendelee na biashara kwa uadilifu,” alisema Ahmad Massoud, mfanyabiashara.
Kwa upande wake, Jessi Joseph kutoka kampuni ya Zanzibar Quality alieleza kuwa wamepokea maagizo hayo na watahakikisha wanafanya biashara ya bidhaa hiyo kulingana na miongozo mipya.
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha usalama wa chakula, kulinda afya ya watoto na kuendeleza ushindani wa haki katika soko.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!