
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa vyama vya wafanyakazi barani afrika kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Amesema kwa kufanya hivyo kutawawezesha kupunguza hatari ya kupoteza ajira kutokana na ujio wa mashine pamoja na matumizi ya teknolojia mpya ikiwemo za akili mnemba.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa 22 Agosti 2025,) Alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika (OAUUT) uliofanyika Hoteli ya Johari Rotana Dar es Salaam.
Amesema kuwa, katika dunia ya sasa, imeshuhudiwa uwepo wa mabadiliko makubwa yanayochagizwa na mapinduzi ya kiteknolojia ikiwemo matumizi ya akili mnemba pamoja na utandawazi.
“Kuna hatari ya watu kupoteza ajira zao kadri mitambo na mifumo ya kisasa inavyochukua kazi ambazo kwa kawaida zingeweza kufanywa na wafanyakazi. Tunapaswa kuweka mpango wa kutoa mafunzo endelevu yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuwandaa wafanyakazi na aina mpya za ajira zinazojitokeza.”
Amesema kuwa Tanzania kwa upande wake chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko hayo ikiwemo kuhamasisha matumizi sahihi ya teknolojia mpya ikiwemo akili mnemba na kusisitiza ulinzi wa haki na faragha za wafanyakazi. “Teknolojia lazima ilinde utu na si kudhoofisha heshima ya kazi.”
Amesema eneo lingine ni kuwajengea uwezo wafanyakazi kupitia programu mbalimbali zitakazowawezesha kuwaongezea ujuzi katika kazi. “Tunafanya hivi ili kuhakikisha watu wetu hasa vijana wanajengewa maarifa na stadi zinazohitajika hasa katika maeneo ya uchumi wa kijani na kidijitali.”
Aidha, amesema Serikali inathamini na kutambua mchango mkubwa wa vyama vya wafanyakazi nchini na itaendelea kushirikiana nao katika kuboresha masilahi ya wafanyakazi.
“Serikali imevipa nafasi vyama vya wafanyakazi kufanya kazi kwa Uhuru na bila kuingiliwa tunawasihi kuendelea kushauriana na kushirikiana na Serikali ili kuendelea kuboresha maslahi na mazingira ya ufanyaji kazi.”
Amesema ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali na vyama hivyo umeiwezesha Serikali kutekeleza mahitaji yote muhimu ya wafanyakazi nchini, ikiwemo maboresho ya Sera, Sheria na maslahi ya wafanyakazi.
Kadhalika, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono jitihada za Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika (OAUUT) ikiwa ni sehemu ya kuenzi jitihada za Baba wa Taifa ambae ni mwanzilishi wa Shirikisho hilo.
Naye Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, amesema Serikali imeendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi nchini na imepitisha Sera na Sheria mbalimbali katika kuhakikisha inarekebisha na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Kwa Upande wake, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika (OATUU), Joshua Ansah amesema chama hicho kitaendelea kusimamia na kuhakikisha kinasimamia maslahi ya wafanyakazi Barani Afrika, ili kuhakikisha usawa na maslahi kwa wafanyakazi wote.
Aidha, ameshukuru viongozi wa vyama vya Wafanyakazi Afrika kwa kuendelea kuunga Mkono Shirikisho hilo katika kufanikisha jitihada za kupigania maslahi ya wafanyakazi.
“Tuendelee kuunga mkono Shirikisho letu kwa Maslahi mapana ya wafanyakazi barani Afrika na pamoja tutaendelea kusimamia na kupigania kuboresha maslahi yao.”
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la wafanyakazi Kanda ya Afrika Mashariki (ILO) Bi. Caroline Mugala, Amesema Chama hicho kitaendelea kusimamia umadhubuti na ufanisi wa vyama vya wafanyakazi ili kuhakikisha Serikali zinaendelea kusimamia maslahi ya wafanyakazi.
“Tunahitaji kuendelea kuwalinda wafanyakazi wetu kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kijamii ikiwemo mazingira na teknolojia ni muhimu wafanyakazi waendelee kupewa mafunzo na kuwezeshwa kukabiliana na mabadiriko haya.”
Amesema ni lazima kila mabadiriko yanayowahusu wafanyakazi yawahusishe wafanyakazi hao na wakubaliane nayo ili kuwa na manufaa kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Tumaini Nyamhokya, amesema chama hicho kinajivunia mafanikio makubwa ambayo kimeyapata kwa kupigania haki za wafanyakazi wote Nchini.
Amesema mafanikio hayo yametokana na mahusiano mazuri ambayo chama hicho kimeyajenga na Serikali pamoja na watumishi jambo ambalo limewezesha chama hicho kufikia malengo yake na kufanya kazi kwa ufanisi
“Tumetumia kwa kiasi kikubwa njia ya majadiliano na maridhiano katika kufanikish mahitaji ya wafanyakazi tunashukuru kwa Upande wetu Serikali yetu imekuwa sikuvu kusikiliza na kutatua changamoto zinazo wakuta wafanyakazi.
Amesema chama hicho kimefurahia kuwa sehemu ya mafanikio na kuhost mkutano Mkuu wa vyama vya wafanyakazi Afrika.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Afrika OATUU lilianzishwa mwaka Aprili 1973 na Rais wa Kwanza wa Tanzania Julius Kambarage Nyerere na Rais wa kwanza wa Ghana Fransis Kwame Nkuruma kwa lengo la kuwaunganisha wafanyakazi na kusimamia maslahi ya wafanyakazi Barani Afrika kwa pamoja.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!