Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Waziri Dkt. Jafo Azindua Rasmi Bodi ya Wajumbe wa TanTrade

  • 1
Scroll Down To Discover

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Seleman Jafo, leo amezindua rasmi Bodi ya wajumbe tisa (9) wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), walioteuliwa hivi karibuni kushika nafasi hiyo muhimu ya uongozi.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Jafo aliwataka wajumbe hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uwazi na uadilifu mkubwa, ili kuiwezesha TanTrade kuwa chombo madhubuti katika kukuza biashara za ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa wajumbe walioteuliwa na kuzinduliwa leo ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Bw. Oscar Kissanga. Waziri Jafo alieleza kuwa uteuzi wa Bw. Kissanga unaleta matarajio makubwa kutokana na uzoefu wake katika sekta ya biashara na ushirikiano wa karibu kati ya TanTrade na TCCIA.

“Ni matumaini yangu kuwa bodi hii mpya itakuwa chachu ya mageuzi na maendeleo katika kukuza biashara na viwanda nchini. Tunahitaji mikakati madhubuti ya kuinua bidhaa zetu katika masoko ya kimataifa na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wetu,” alisema Dkt. Jafo.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa bodi hiyo kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika maonesho ya kibiashara ndani na nje ya nchi, pamoja na kuboresha mfumo wa taarifa za soko kwa wajasiriamali na wawekezaji.

Wajumbe wengine walioteuliwa kwenye bodi hiyo wanawakilisha taasisi mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, wakitarajiwa kuleta mchanganyiko wa utaalamu na uzoefu unaohitajika kuendeleza dhamira ya serikali ya kukuza uchumi wa viwanda kupitia biashara.

Naye Mjumbe mpya wa bodi hiyo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya biashara,Viwanda na Kilimo Tanzania(TCCIA) Bw. Oscar Kissanga alisema anamshukuru Mhe. Waziri wa Biashara na Viwanda Dkt.Seleman Jafo kwa kumwamini na kumteua kuwa mmoja wa wajumbe kati ya(9).

“Uzinduzi huu wa bodi ya TanTrade ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika kukuza biashara na viwanda nchini. Kama TCCIA, tumejipanga kushirikiana kikamilifu na bodi hii kuhakikisha fursa za biashara, hasa kwa wajasiriamali wa ndani, zinapanuliwa na zinatumika kikamilifu katika soko la ndani na la kimataifa.” alisema Kissanga



Prev Post Chid Benz Arejeshewa Tabasamu Awaasa Wasanii Kukaa Mbali Na Dawa Za Kulevya
Next Post Majaliwa: Tuwawezeshe Wafanyakazi Kukabiliana na Mabadiliko ya Teknolojia
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook