

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Aprili 27, 2025, ameweka hadharani ujumbe wa baraka alioupokea kutoka kwa hayati Papa Francisko, siku chache kabla hajaitwa na Mungu.
Kupitia kurasa zake rasmi za X na Instagram, Rais Samia ameeleza kwa unyenyekevu na shukrani kuu jinsi alivyopokea barua hiyo, iliyomfikishwa na Askofu Mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican hapa nchini. Katika ujumbe wake, Papa Francisko alimpongeza Rais Samia pamoja na Watanzania wote kwa maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika Aprili 26, 2025.
Rais Samia ameandika:
“Kwa unyenyekevu na shukrani, nimepokea ujumbe wa hayati Papa Francisko kwangu, kwa nchi yetu na kwa Watanzania wote, aliouandika siku chache kabla Mwenyezi Mungu hajamwita kwake. Tuendelee kumwombea alale mahali pema.”
Itakumbukwa kuwa wakati wa mazishi ya Papa Francisko yaliyofanyika Vatican, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango alieleza kuwa barua hiyo ni miongoni mwa nyaraka za mwisho kabisa alizosaini Papa huyo mtakatifu, akionesha upendo na heshima kwa taifa la Tanzania.
Kwa Watanzania, ujumbe huu wa baraka kutoka kwa Papa Francisko unabeba uzito mkubwa, ukiwa ni alama ya upendo wa kiroho na mshikamano wa kimataifa katika kipindi hiki cha maombolezo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!