
Familia ya mwigizaji na gwiji wa sanaa za mapigano, Chuck Norris, imekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni zikidai kifo chake, zikieleza kuwa zimejaa upotoshaji unaotokana na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI).
Kupitia taarifa yao ya umma, familia hiyo imesema kuwa machapisho na video mbalimbali zinazozunguka mitandaoni kuhusu afya, mazingira ya kifo na historia ya maisha yake ni za uongo na hazina ukweli wowote. Wameeleza kuwa baadhi ya taarifa hizo zimefikia hatua ya kubuni maelezo ya kitabibu na simulizi zisizo sahihi kuhusu familia yake.
Familia hiyo imewahimiza mashabiki na umma kwa ujumla kutopokea wala kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho, wakisisitiza kuwa taarifa sahihi zinapaswa kupatikana kupitia vyanzo rasmi vya familia au wawakilishi wake.
Wameongeza kuwa ingawa taarifa kuhusu maisha binafsi na hali ya afya ya Norris zimekuwa zikishughulikiwa kwa uangalifu na faragha, wameendelea kutoa heshima kwa mashabiki wanaoendelea kumuenzi kupitia kazi zake na mchango wake katika tasnia ya burudani.
Chuck Norris amekuwa jina kubwa duniani kupitia filamu za mapigano na vipindi vya televisheni, ikiwa ni pamoja na Walker, Texas Ranger, pamoja na historia yake katika sanaa za mapigano na umaarufu wa mitandaoni kupitia “Chuck Norris facts” ambazo zilimfanya kuwa nguli wa utani wa mtandaoni.
Familia yake kwa sasa inaendelea kusisitiza umuhimu wa kuheshimu taarifa sahihi na kupuuza uvumi unaosambazwa bila uthibitisho, huku zikizidi kuibua mjadala kuhusu athari za taarifa potofu zinazoenezwa na teknolojia ya AI kwenye mitandao ya kijamii.
The post AI Yaibua Taarifa za Uongo Kuhusu Chuck Norris, Familia Yatoa Tamko appeared first on Global Publishers.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!