

Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wakili Gaston Garubindi, amethibitisha kuwa maombi ya Habeas Corpus kwa ajili ya kuiomba Mahakama iagize Jeshi la Polisi kumfikisha Mahakamani au kumpatia dhamana Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Tanzania Bara, John Heche, yamefunguliwa rasmi Mahakamani.
Kupitia taarifa iliyotolewa Alhamisi, Novemba 6, 2025, Wakili Garubindi amesema maombi hayo yamesajiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, na yamepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Obadia Bwegoge.
Kwa mujibu wa maelezo yake, kwa sasa wanasubiri summons kwa ajili ya wajibu maombi ambao ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na maofisa wengine watano.
Amefafanua kuwa maombi hayo mapya yamewasilishwa baada ya yale ya awali yaliyowasilishwa Dodoma kukumbwa na changamoto ya mtandao, huku Heche akidaiwa kusafirishwa kutoka Dodoma kurejeshwa Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Heche ameshikiliwa na Polisi tangu tarehe 22 Oktoba 2025 alipokamatwa na kudaiwa kusafirishwa Tarime, lakini baadaye ikabainika hakupelekwa huko kama tulivyofahamishwa. Baada ya jitihada mbalimbali, tulibaini alikuwa anashikiliwa Kituo cha Polisi Mtumba jijini Dodoma bila dhamana wala kufikishwa Mahakamani,” alisema Wakili Garubindi.
Ameongeza kuwa Heche alisafirishwa tena kutoka Dodoma kupelekwa Dar es Salaam, na maombi ya Habeas Corpus yamewasilishwa rasmi Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam.
Wakili Garubindi amesema CHADEMA itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya maombi hayo yanayolenga kuhakikisha haki za Makamu Mwenyekiti wao zinaheshimiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!