
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma, leo Jumatano Oktoba 15, 2025, imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa na Luhaga Mpina na chama cha ACT-Wazalendo kupinga uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wa kumuengua Mpina katika nafasi ya kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Fredrick Manyanda, likisaidiwa na Majaji Sylvester Kainda na Abdallah Gonzi, limeeleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za Uchaguzi, NEC ni chombo huru kisichopaswa kuingiliwa na mahakama au taasisi nyingine endapo limefanya maamuzi yake kwa nia njema na kwa kufuata taratibu.
Mahakama imeeleza zaidi kuwa hoja zilizowasilishwa na upande wa walalamikaji hazikuonyesha ukiukwaji wa haki za msingi wala ushahidi wa upendeleo katika mchakato wa kuenguliwa kwa Mpina.
Kwa uamuzi huo, Luhaga Mpina hataweza kushiriki katika kinyang’anyiro cha urais mwaka huu, huku kampeni za vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo zikiendelea kote nchini.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!