
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeahirishwa leo Jumatano, Oktoba 15, 2025, kufuatia kifo cha Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Asha Mwetindwa.
Kesi hiyo, ambayo inasikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, chini ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Danstan Ndunguru, ilipangwa kuendelea leo kwa mshtakiwa kuendelea kumuhoji kwa maswali ya dodoso (cross examination) shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri, Inspekta wa Polisi John Kaaya.
Hata hivyo, baada ya kesi kuitwa majira ya saa 3:00 asubuhi, Wakili wa Serikali Mkuu Renatus Mkude, ambaye ni kiongozi wa jopo la Mawakili wa Jamhuri, aliieleza Mahakama kuhusu msiba huo na kuomba kesi iahirishwe ifikapo saa 5:00 asubuhi ili kutoa nafasi kwa mawakili wa Serikali kushiriki katika ibada ya mazishi ya marehemu, ambayo yamepangwa kufanyika Kisemvule, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.
Hakukuwa na pingamizi kutoka kwa upande wa mshtakiwa, ambapo Lissu alitumia fursa hiyo kutuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na wote watakaoshiriki maziko ya marehemu. Baada ya hapo, Mahakama iliendelea kwa muda mfupi kabla ya kuahirisha rasmi mwenendo wa kesi hiyo.
Kesi hiyo sasa itaendelea tena kesho, Alhamisi Oktoba 16, 2025, ambapo Tundu Lissu ataendelea kumuhoji shahidi huyo wa upande wa Jamhuri.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!