

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) limekanusha vikali taarifa inayosambaa mitandaoni ikidai kuwa ni tamko rasmi la baraza hilo kuhusu amani ya taifa kuelekea uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kanusho iliyotolewa leo, Jumatatu Oktoba 13, 2025, na Katibu Mkuu wa TEC, Padri Dkt. Charles Kitima, imeelezwa kuwa baraza hilo halijawahi kutoa waraka wowote wa aina hiyo, na kwamba maudhui yanayosambazwa hayana uhusiano wowote na msimamo wa TEC.
“Tunapenda kuwatangazia waumini na Watanzania wote kwa ujumla kuwa waraka huo haukutolewa na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania,” alisema Padri Dkt. Kitima.
Aidha, Padri Kitima amewataka wananchi kuwa makini na taarifa zinazochapishwa au kusambazwa mitandaoni, akisisitiza umuhimu wa kuthibitisha chanzo cha habari kabla ya kuziamini au kuzitumia.
“Ni vyema wananchi wakawa waangalifu na taarifa zisizo rasmi, kwani zinaweza kusababisha taharuki au kupotosha umma, hasa katika kipindi nyeti kama hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu,” aliongeza.
TEC imeeleza kuwa endapo kutakuwa na taarifa au tamko lolote rasmi la baraza hilo, litawasilishwa kupitia vyombo vya habari vya kanisa na njia rasmi za mawasiliano.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!