
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025 Bw. Ismail Ali Ussi amewataka wananchi wa Manispaa ya Morogoro na Mkoa huo kwa jumla kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji ili miundombinu hiyo iwezekutumika kwa muda mrefu.
Wito huo umetolewa na kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru wakati anazindua mradi wa ujenzi wa Birika la maji lenye ujazo wa lita 1,000,000 uliopo katika manispaa ya Morogoro unaotekelezwa chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA).
Bw. Ussi amesema kuna ulazima wa wananchi wa Mkoa huo kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake katika kutunza miundombinu ya miradi ya maji kwa sababu Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu hiyo.
“… Niwaombe sana wananchi wa eneo hili muendelee kuitunza miundombinu hii ya maji ambayo mnapatiwa na Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Bw. Ussi Aidha kiongozi huyo amewataka viongozi wa Serikali katika Halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia kikamillifu miundombinu hiyo ya maji na kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa wakati uliokusudiwa ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwanalisa Mshana mkazi wa Kata ya Kiegea ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za mradi huo ambao utaenda kuondoa adha ya maji ambapo awali walikuwa wakikumbana nazo huku akitoa ombi la kuongezewa siku za kupata maji kutoka siku moja hadi mbili kwa wiki.
Mradi wa ujenzi wa Birika la Maji lenye ujazo wa Lita milioni moja umegharimu zaidi ya shilingi milioni 46.8 ambapo unatarajiwa kutoa huduma kwa wananchi waishio Mitaa isiyopungua sita ya Nguvukazi, Kiegea A, Kilimanjaro, Yespa na Kihonda Kaskazini katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!