

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Nyamagana, Ezekia Wenje, amejiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kueleza kuvutiwa na kazi kubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Wenje ametangaza uamuzi huo leo, Oktoba 13, 2025, katika mkutano wa kampeni za mgombea urais wa CCM uliofanyika wilayani Chato, mkoani Geita, ambapo alihudhuria kama mgeni maalum.
Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa wananchi, Wenje alisema amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina kuhusu mustakabali wa taifa na kuona umuhimu wa kulinda amani, ambayo alisema ndiyo nguzo kuu ya maendeleo.
“Nimeamua kujiunga na CCM kwa sababu nimeona dhamira ya kweli ya serikali ya Dk. Samia katika kulinda amani na kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli. Amani ndiyo msingi wa maendeleo, na siwezi kuunga mkono harakati za kuvuruga hali hiyo,” alisema Wenje.
Wenje aliongeza kuwa amevutiwa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), maboresho ya miundombinu ya barabara, huduma za afya, elimu, na upatikanaji wa maji safi vijijini.
“Serikali hii inafanya kazi kubwa, miradi inaonekana kila kona. Nimeona ni heri niwe sehemu ya wale wanaounga mkono juhudi hizi badala ya kupinga kila kitu,” aliongeza.
“Sijaja hapa kwa chuki, nimekuja kwa sababu ya imani yangu kwa mustakabali wa taifa. Lakini napenda kusema wazi si kweli kwamba CHADEMA imezuiliwa kushiriki uchaguzi. Hizo ni propaganda,” alisema.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!