
Zanzibar, 12 Oktoba 2025
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameizindua rasmi Jumuiya ya Wakandarasi wa Sekta ya Ujenzi Zanzibar na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta hiyo kutokana na umuhimu wake katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Serikali.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jumuiya hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi, tarehe 12 Oktoba 2025.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya ujenzi katika miaka ya karibuni kwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, skuli na hospitali.
Amesema kuanzishwa kwa jumuiya hiyo kutatoa fursa ya ushirikiano, mijadala na kubadilishana taaluma baina ya Serikali na wadau wa sekta hiyo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza hatua ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo, akibainisha kuwa ni chombo muhimu cha kuwasilisha changamoto, ushauri na mapendekezo kwa Serikali yatakayosaidia kuimarisha sekta ya ujenzi nchini.
Halikadhalika, ameleezea kuwa sekta ya ujenzi Zanzibar sasa imefungua ukurasa mpya wa historia kwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta hiyo katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wadau hao kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na jumuiya hiyo ili kuhakikisha inaendelea kutoa mchango wake katika kukuza sekta ya ujenzi na sekta nyengine za uchumi.
Kuhusu changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa wadau wa sekta hiyo, Dkt. Mwinyi ameziagiza Wizara ya Ujenzi pamoja na Bodi ya Wakandarasi kuhakikisha zinawaunganisha wadau hao na taasisi za kifedha ili waweze kupata mikopo, sambamba na kuangalia uwezekano wa kuanzisha mifuko maalum ya kuwasaidia.
Vilevile , Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa umoja, mshikamano na kuepuka migogoro isiyo na tija miongoni mwa wadau hao, akibainisha kuwa ushirikiano wao ni muhimu katika kuleta maendeleo endelevu ya sekta ya ujenzi Zanzibar.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!