Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Polisi Arusha Washikilia Watu 5 Kufuatia Mauaji ya Askari Omary Mnandi – Video

  • 4
Scroll Down To Discover

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji ya Askari Polisi, Omary Mnandi (30), ambaye alikuwa mkazi wa Jiji la Arusha.

Akizungumza na vyombo vya habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 12, 2025, katika baa inayojulikana kwa jina la Simaloi, iliyopo maeneo ya Kaloleni, jijini Arusha.

Kwa mujibu wa Kamanda Masejo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo kilikuwa ni mkanganyiko uliosababishwa na hali ya ulevi wa marehemu, ambapo alikosea kuingia kwenye gari lisilo lake gari lenye namba T. 734 AXR — ambalo lilikuwa jirani na lake lenye namba T. 402 CNC. Watuhumiwa walipomkuta akiwa amelala ndani ya gari hilo, walimshambulia kwa kipigo kikali na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimbali za mwili.

“Marehemu alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kutokana na majeraha aliyopata,” alisema SACP Masejo.

Mashuhuda wa tukio hilo, ambao hawakutaka kurekodiwa rasmi, wamelieleza Jambo TV kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa sita usiku. Wanasema kuwa marehemu, akiwa amelewa kupita kiasi, alichanganya magari na kuingia katika gari la watu wengine ambapo alilala usingizi mzito ndani yake. Wamiliki wa gari hilo waliporejea muda mfupi baadaye, walipatwa na taharuki walipomkuta mtu asiyejulikana akiwa amelala ndani ya gari lao, na ndipo walipochukua sheria mkononi kwa kumpiga vibaya wakidhani ni mwizi

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi wa kina wa tukio hilo, na baada ya kukamilika kwa hatua za awali za upelelezi, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote wanaohusika.



Prev Post Maelfu Wamiminika Kumsikiliza Dkt. Samia Mbogwe, Geita
Next Post Mgombea Urais Dkt. Samia Aahidi Kuimarisha Madini na Upatikanaji wa Maji Mbogwe, Geita
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook