Na Silivia Amandius.
Bukoba, Kagera.
Katika kuadhimisha miaka 25 ya huduma kwa wakulima na wafugaji, PASS Trust imeandaa jukwaa maalum lenye lengo la kuimarisha ushirikiano na taasisi za fedha nchini, ili kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wadau wa sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu.
Akizungumza katika semina iliyowakutanisha wadau wa sekta hizo, Mkurugenzi wa Biashara wa PASS Trust, Bw. Adam Kamanda, amesisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha kuendelea kushirikiana na PASS Trust katika kufungua fursa zaidi za uwezeshaji kwa wakulima, hususan wale wanaojihusisha na uzalishaji wa mazao katika Kanda ya Ziwa.
“Taasisi za kifedha zina nafasi ya kipekee katika kusaidia wakulima kuongeza tija na thamani ya uzalishaji. Kupitia ushirikiano na PASS, tunaweza kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuwapa mitaji wanayohitaji kwa masharti nafuu,” amesema Bw. Kamanda.
Aidha, amebainisha kuwa jukwaa hilo ni sehemu ya juhudi endelevu za PASS Trust kuhakikisha wakulima wadogo na wakubwa wanakuwa sehemu ya uchumi jumuishi na endelevu.
Kwa mujibu wa PASS Trust, lengo kuu la jukwaa hilo ni kujenga majadiliano yenye tija kati ya taasisi za kifedha na wadau wa kilimo, ili kuibua mbinu bora za kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa sekta zisizo rasmi — sekta ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto za mitaji.
Jukwaa hilo limeelezwa kuwa ni miongoni mwa matukio muhimu katika maadhimisho ya miaka 25 ya PASS Trust, likiwa kielelezo cha dhamira ya taasisi hiyo kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na wadau mbalimbali kwa ajili ya kukuza sekta ya kilimo nchini.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!