
Dar es Salaam, Oktoba 10, 2025 — Kuanzia Oktoba 23, 2025, Watanzania wanaoomba viza za utalii au biashara kwenda Marekani watahitajika kuweka dhamana ya kifedha (visa bond) itakayokuwa kati ya dola 5,000, 10,000 au 15,000 za Kimarekani, kulingana na uamuzi wa ubalozi wa Marekani.
Kiasi hicho cha dhamana hakihusiani na ada ya kawaida ya maombi ya viza, bali ni hatua ya ziada inayolenga kudhibiti tabia ya baadhi ya waombaji wanaobaki Marekani kinyume cha sheria baada ya muda wa viza zao kumalizika.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Marekani, fedha hiyo itarudishwa endapo mwombaji atarejea Tanzania ndani ya muda halali wa viza yake. Hata hivyo, ikitokea amevuka muda wa viza (overstay), dhamana hiyo haitarejeshwa.
Hatua hii ni sehemu ya sera mpya za udhibiti wa uhamiaji zinazotekelezwa na Serikali ya Marekani kwa nchi ambazo raia wake wamekuwa wakionekana kukiuka masharti ya viza mara kwa mara.
Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kujadiliana na Marekani kuhusu masharti hayo mapya, ikilenga kuhakikisha kwamba Watanzania wanaosafiri kwa nia halali hawataathirika na uamuzi huo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!